Musoma Vijijini wamweleza Prof.Muhongo wapo tayari kuhesabiwa wote ili kujumuishwa katika mipango ya maendeleo

NA FRESHA KINASA

KAMPENI ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoa Mara ambayo imefanywa na Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo imefanikiwa kwa asilimia 100 ambapo wananchi jimboni humo wameelimishwa kwa kina juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. 

Hivyo wamesema wamejitayarisha kuhesabiwa wote ili kuipa nafasi Serikali Kuu iweze kuwaandalia mipango jumuishi na shirikishi ya maendeleo.
Ambapo Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mheshimiwa Prof. Muhongo ameweza kufikisha elimu hiyo katika vitongoji, vijiji na visiwa ikiwemo Kisiwa cha Rukuba na kwamba wananchi wote wamehamasika sana kushiriki kuhesabiwa siku ya sensa Agosti 23, 2022 kwa maendeleo yao na taifa.

Wakati wa Kampeni hiyo ya kutoa elimu na hamasa jambo jema na zuri ni kwamba wananchi walipewa fursa ya kuuliza maswali ambayo yalifanunuliwa na viongozi mbalimbali pamoja na Mbunge Mheshimiwa Prof. Muhongo na kuwapa uelewa wa kina juu ya zoezi hilo muhimu kwa nchi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini wakati akitoa elimu na hamasa kwa wnaanchi jimboni humo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Makarani watakaopita wakitekeleza jukumu hilo Agosti 23, 2022.
Aidha Mheshimiwa Prof. Muhongo akizungumzia na Wananchi wa Visiwa vya Rukuba na Iriga wakati wa Kampeni ya kutoa elimu na hamasa kwa Wananchi wa Visiwa hivyo ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini amesema, "Na Mimi Mwenyewe tarehe 23, 2022 kwa kuwa ni raia mwema najipenda, napenda Jimbo langu la Musoma, napenda taifa langu Tanzania itabidi nitulie nyumbani nisubiri kuhesabiwa, ndugu zangu nawaomba sana tuhesabiwe wote kwa asilimia 100,"amesema Prof. Muhongo.

Kwa upande wao wananchi wamesema kuwa, elimu waliyoipata imewapa mwanga na upeo mkubwa juu ya umuhimu wa sensa na kwamba wamejiandaa kuhesabiwa kwa asilimia 100 katika kuhakikisha kwamba serikali inapata takwimu sahihi zitakazo iwezesha kuwahudumia na kupanga mipango ya maendeleo.
"Mbunge Mheshimiwa Prof. Muhongo ameshiriki kikamilifu kutuelimisha na pia tumepata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo pia majibu yalitolewa kwa ufafanuzi wa kina, kilichopo ni kuhesabiwa kwa manufaa yetu na Taifa letu, maana tuna uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na tumehamasika sana kuhesabiwa,"amesema Paul.

Post a Comment

0 Comments