Naibu Waziri Masanja akagua Mradi wa Kitalu cha Miche ya Miti wilayani Magu

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amekagua mradi wa kitalu cha miche ya miti wenye thamani ya shilingi milioni 43 unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (wa pili kutoka kulia) akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali(aliyeinama) kukagua mradi wa kitalu cha miche ya miti kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Wengine ni Maafisa wa TFS pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wilaya ya Magu.

Akizungumza leo katika ziara, Mhe. Masanja amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuitunza miche ya miti watakayokabidhiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili iweze kuleta matokeo chanya ya kuhifadhi mazingira.

“Tuwaombe wananchi miche hii watakapogawiwa waitunze vizuri kwa ajili ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo,”Mhe. Masanja amesisitiza.

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, awamu ya kwanza zimetolewa fedha kiasi cha shilingi milioni 17 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ambapo Serikali itaendelea kutoa fedha kwa awamu nyingine ili kukamilisha mradi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(wa pili kutoka kulia) akitoa maelekezo kuhusu kusimamia vizuri mradi wa kitalu cha miche ya miti kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakati za ziara yake ya kikazi leo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali na wengine ni Maafisa wa TFS pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wilaya ya Magu.

Ameongeza kuwa lengo la uanzishwaji wa kitalu hicho ni kupunguza athari za uharibifu wa mazingira hususan katika Mkoa wa Mwanza ambapo kwa sasa utekelezaji wake umeanzia Wilaya ya Magu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum Kali amesema kupitia kitalu hicho wananchi wa Wilaya ya Magu watanufaika sana kwa sababu miche itapelekwa kwenye maeneo ambayo yalikwishaharibika ili kuyarudisha kwenye asili yake ya awali.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(kulia) moja ya miche ya parachichi inayopatikana katika kitalu cha miche ya miti kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Wengine ni watendaji kutoka Wilaya ya Magu.  

Aidha, Mhe. Kali ametoa rai kwa wananchi kuitunza na kuilinda miche ya miti watakayokabidhiwa .

“Kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake na kwa wale wafugaji msiingize mifugo kwenye maeneo ambayo tumepanda miti”amesema Mhe. Kali.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Kanda ya Ziwa, Thomas Moshi amesema kitalu hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha miche laki tatu kwa mwaka, hivyo kuendelea kuihudumia jamii ili kuhakikisha maeneo ambayo hayana miti uoto wa asili unarudi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(kulia) akikagua miche ya miti katika kitalu kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakati za ziara yake ya kikazi leo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali na wengine ni Maafisa wa TFS pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wilaya ya Magu.

Amesema, wananchi wanatakiwa kuelimishwa ili waweze kujua faida za miti katika kuleta nishati mbadala, kuleta mvua na pia kutumika kama mitishamba ya dawa za asili.Kitalu hicho kimefadhiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Mfuko wa Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) baada ya kukagua mradi wa kitalu kinachosimamiwa na leo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news