Prof.Herath:Mafisadi walioumiza uchumi wa Sri Lanka watalipa gharama

NA GODFREY NNKO

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma ya Bunge (COPE) nchini Sri Lanka, Prof. Charitha Herath amesema kuwa, ingawa kuahirishwa kwa Bunge kulisababisha kuvunjika kwa kamati ya uangalizi hakupaswi kuzuia uchunguzi uliopangwa kubaini waliohusika na mdororo wa kiuchumi nchini humo.
Prof. Herath amesema kuwa, COPE ilikuwa katika hatua za mwisho kuanzisha uchunguzi kwa ajili ya kuwasilisha ripoti ngazi husika kulingana na matakwa ya kisheria,hivyo mafisadi wote waliohusika kutafuna fedha za Sri Lanka hadi kusababisha uchumi wake kudorora lazima wasakwe.

Hayo yanajiri huku Sri Lanka ikiwa tayari ina Rais mpya Ranil Wickremesinghe ambaye wabunge walimchagua kwa wingi wa kura kukamilisha muhula uliosalia wa Rais Gotabaya Rajapaksa wa miaka mitano utakaofikia kikomo mwaka 2024, ambapo alishinda katika uchaguzi wa urais wa Novemba 2019.

Rais Rajapaksa aliikimbia nchi baada ya mdororo mkubwa wa kiuchumi ambao ulisababisha wananchi kuingia mitaani, hivyo Bunge lilipiga kura ambazo zilizokuwa na ushindani, ambapo Wickremesinghe alipata kura 134 huku mpinzani wake mkuu Dulla Alahapperuma akijizolea kura 82.

Mgombea wa tatu, Anura Kumara Dissanayake, alipata kura tatu pekee kutoka kwa chama chake. Rais wa zamani Gotabaya Rajapaksa alimteua Wickremesinghe kama waziri mkuu mwezi Mei,mwaka huu akitarajia uteuzi huo ungeleta utulivu katika nchi hiyo ambayo inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Wickremesinghe alihudumu kama rais wa mpito baada ya Rajapaksa kuikimbia nchi hiyo na kujiuzulu kwa njia ya barua pepe.

Katika mahojiano na The Island, Prof. Herath ambaye pia ni Mbunge nchini Sri Lanka amesema, kutokana na hali hiyo, hakufanya kazi tena kama Mwenyekiti wa COPE.

Amesema, kamati zote, isipokuwa Kamati Kuu inayoongozwa na Spika Mahinda Yapa Abeywardena, Kamati za Kusimamia Sekta na Kamati Teule za Bunge zilivunjwa,hivyo anaona kuna haja ya mamlaka kutoa nafasi ili uchunguzi uweze kuendelea dhidi ya waliohusika na mdororo wa uchumi.

"Uchunguzi unaopendekezwa utatokana kwa kiasi kikubwa na ripoti iliyopokelewa na Bunge kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, W.P.C. Wickremeratne wiki kadhaa zilizopita,"Prof. Herath alisema.

Prof.Herath alisema kuwa, shirika hilo la uangalizi wa bunge aliloliongoza lilipanga vikao vyake vya kila siku kwa muda wa wiki mbili ili kuchunguza msururu wa masuala ambayo hatimaye yalipelekea tamko lililotolewa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Dkt.Nandalal Weerasinghe tarehe 19 Mei, kwamba nchi haikuwa na uwezo wa kulipa deni lake la nje.

"Hii ilikuwa wiki moja baada ya kiongozi wa UNP Ranil Wickremesinghe kukubali uwaziri mkuu," Prof. Herath alisema, huku akisisitiza jukumu la Bunge kufanya upigaji kura kuzuia uchunguzi wa suala zima.

Taarifa za awali bungeni zilionesha kuwa, uchunguzi huo ungeanzishwa Julai 19, lakini haukuweza kutokana na msukosuko wa kisiasa, uliosababishwa na kulazimishwa kujiuzulu kwa Rais Gotabaya Rajapaksa.

Miongoni mwa walioombwa kufika mbele ya kamati ya bunge ni Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Nandalal Weerasinghe, na watangulizi wake, Prof. W.D. Lakshman (Desemba 2019-Septemba 2021) na Ajith Nivard Cabraal (Septemba 2021-Machi 2022), Katibu wa Rais wa zamani, Dkt.P.B. Jayasundera (Novemba 2019-Desemba 2021), Katibu wa Fedha Mahinda Sirisiwardana na watangulizi wake, S.R. Attygalle na Dk. S.R. Samarasinghe, ambaye sasa anafanya kazi kama mshauri wa Rais Ranil Wickremesinghe.

COPE pia ilipanga kuwaita wanachama wa zamani wa Bodi ya Fedha, Sanjiva Jayawardena, PC, na Dk.Ranee Jayamaha na wengine. Gavana, CBSL na Katibu wa Hazina ni wajumbe wa Bodi ya Fedha kwa nafasi zao.

Alipoulizwa kama angependa kuteuliwa tena kuwa Mwenyekiti wa COPE, Prof. Herath alisema kuwa, yuko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika kwake, hasa dhidi ya hali ya nyuma ya hakikisho la Rais Wickremesinghe kwa Bunge kuhusu kampeni ya hali ya juu dhidi ya ufisadi.

Prof.Herath alimnukuu Rais Wickremesinghe wakati akilihutubia Bunge akisema kuwa: “Ni muhimu kuondoa kabisa hongo, rushwa na udanganyifu katika jamii yetu. Nitatekeleza sera ya taifa ya kupambana na rushwa na ufisadi. Sheria na kanuni na amri mpya katika suala hili zinatayarishwa na Wizara ya Sheria. Makubaliano yatafikiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa kuhusu kupambana na rushwa."

Prof. Herath alisisitiza kuwa, bila kujali maafikiano kuhusu masuala ya kisiasa, mzozo uliopo haungeweza kutatuliwa isipokuwa hatua madhubuti zichukuliwe ili kuadhibu wote pia kuzuia vitendo vya rushwa vinavyohusisha sekta ya umma na binafsi.

Aidha, Prof. Herath alisema kuwa, wale ambao wanaweza kutoa taarifa zinazohusiana na uchunguzi huo, watapewa fursa ya kufanya hivyo.

Wakati huo huo, ameieleza The Island kuwa, huenda hata asifikiriwe kuteuliwa tena kuwa Mkuu wa COPE kutokana na yeye kujiunga na kundi upinzani ambalo lilimuunga mkono Dullas Alahapperuma, kwenye kinyang'anyiro cha urais.

Prof. Herath alisisitiza kuwa ana uhakika msimamo wake wa kisiasa haupaswi kuwa kigezo cha kunyimwa nafasi ya kuhudumia umma.

Prof. Herath alisema kuwa nchi haiwezi kusonga mbele bila kubaini ni nani aliyeleta janga hilo katika nchi yao. Amesema kuwa, mikakati ya zamani ya kisiasa haitakuwa na umuhimu katika muktadha wa sasa, huku akifafanua kuwa,hakuna mtu anayeweza kupinga mchakato uliopitishwa katika uchaguzi wa Rais Wickremesinghe kama Rais wa Nane.

Taifa la Sri Lanka limekosa fedha za kulipia uagizaji bidhaa za kimsingi na mahitaji kama vile chakula, mbolea, dawa na mafuta na kusababisha takribani watu mioni 22 wa taifa hilo la kisiwa kukata tamaa.

Aidha, kushuka kwa kasi kwa uchumi wake kunashangaza kwani kabla ya mgogoro huu, uchumi wa Sri Lanka ulikuwa umeimarika na tabaka la kati lilikuwa katika hali nzuri.

Pia kabla ya kufikia hatua ya mzozo huo mkubwa,Serikali ya Sri Lanka ilikuwa imeanza majadiliano ya awali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu mkopo wa uokozi ili kuwakwamua katika hali mbaya ya kiuchumi, lakini majadiliano hayo yalisambaratishwa na machafuko dhidi ya serikali.

Msemaji wa IMF, Gerry Rice aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa, wafanyakazi wa hazina hiyo walikuwa bado wanawasiliana na maafisa wa serikali ya ngazi ya kiufundi na wanatarajia kuanza tena mazungumzo mara tu itakapowezekana ili kuondokana na mdororo mbaya wa kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news