Rais Dkt.Mwinyi amwelekeza Balozi Dkt.Haji kuzingatia mambo muhimu kwa manufaa ya Watanzania

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Mwinyi amezungumza na Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt.Suleiman Haji aliyefika Ikulu kumuaga. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa nchini Marekani, Mhe Suleiman Haji Suleiman baada ya kumaliza mazungumzo yao alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ikulu. (Picha na Ikulu).

Kupitia mazungumzo hayo ya Agosti 4, 2022 Ikulu jijini Zanzibar, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemtaka Balozi huyo kuangalia fursa zitakazopatikana katika kituo chake cha kazi na kusaidia kuinua uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo ya uwekezaji pamoja na ile ya kujenga uwezo.

Amesema, kituo hicho kina fursa pana kutokana na kutembelewa na watu kutoka mataifa mbalimbali Duniani, hivyo akamtaka kuikumbuka Zanzibar kwa jicho la pekee.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefarijika sana na Uwakilishi wa Balozi huyo katika kituo hicho.

Mapema, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt.Suleiman Haji aliahidi kutumia nguvu, maarifa na juhudi zake zote ili kutekeleza vyema majukumu yake na kuiletea Maendeleo Tanzania.

Alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi kwa uteuzi wake wa kushika wadhifa huo.

Katika hatua nyingine akizungumza na waandishi wa habari, Mwakilishi huyo ambaye muda mfupi ujao anatarajiwa kuripoti katika Kituo chake cha kazi jijiji New York Marekani, alisema kituo hicho kina fursa nyingi zinazoweza kuinufaisha Tanzania endapo zitatumika vizuri, ikiwemo suala la ufadhili katiika sekta ya Uchumi wa Buluu ambapo wavuvi, wafanya biashara na wakulima wa mwani wataweza kunufaika.

Alilitaja eneo jingine ambalo Zanzibar, ikiwa nchi ya Kisiwa itaweza kunufaika ni upatikanaji wa fedha katika kukabiliana na athari za kimazingira, akibainisha maeneo mbali mbali ya Visiiwa vya Unguja na Pemba kukabiliwa na hali mbaya ya kimazingira kutoka na uvamizi wa maji chumvi.

Aidha, alisema anakusudia kufanya juhudi ili kuhakikisha Watalii wa madaraja ya juu kutoka Marekani wanakuja nchini, na hivyo akatumia fursa hiyo kuitaka Serikali kujipanga kwa kuwa na miundo mbinu bora ili kuvutia watalii hao.
Balozi Suleiman alisema kuwa, Watanzania wana fursa pana ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Marekani kwa kuzingatia uwepo wa Vyuo vikuu kadhaa vinavyohitaji huduma hizo, hivyo akaiomba Serikali kupitia Baraza la kiswahili (BAKIZA) kujidhatiti katika suala la kuzalisha walimu wengi wenye uwezo wa kufundisha lugha hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news