Rais Dkt.Mwinyi azipongeza taasisi zisizo za kiserikali kwa mchango wao huduma za kijamii

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema ushiriki wa taasisi zisizo za kiserikali katika uimarishaji wa huduma za kijamii ni muhimu, kwa kuzingatia kuwa Serikali haina uwezo wa kuwafikia wananchi wote.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na ujumbe wa Taasisi ya Zanzibar Milele Foundation ulipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo leo.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar leo Agosti 30, 2022 alipozungumza na viongozi wa taasisi za Milele Zanzibar Foundation na IFRAJ waliofika kumsalimia pamoja na kuelezea kwa kina shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hizo.

Amesema, kwa kipindi kirefu sasa taasisi hizo zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kuisaidia Serikali, hususani katika uimarishaji wa sekta za huduma ya jamii.

Amezipongeza taasisi hizo kwa kufanya kazi kubwa na kuwa taasisi zinazofanya vyema zaidi hapa nchini katika kuisaidia Serikali katika uimarishaji wa sekta za huduma za jamii, ikiwemo afya, elimu, maji na uwezeshaji wajasiriamali.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza akiwa miongoni mwa ujumbe wa Taasisi ya Zanzibar Milele Foundation ulipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo leo.

“Ninaridhika na kazi kubwa mnayofanya kwa kuwa inagusa vipaumbele vya Serikali katika kuimarisha huduma za kijamii,”amesema.

Ameeleza kufurahishwa kwake na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hizo katika kujenga mifumo pamoja na kuzingatia umuhimu wa ujenzi wa miundombinu, uwepo wa rasilimali watu na mahitaji ya vifaa katika sekta hizo.

Dkt.Mwinyi alieleza kuwa Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama, hivyo hatua inayochukuliwa na taasisi hizo ya kusaidia upatikanaji wa pampu pamoja na uchimbaji wa visima ni ya kupongezwa.

Alipongeza taasisi ya IFRAJ kwa ujenzi wa nyumba 500 za makazi ya binadamu na kusema hatua hiyo ni muhimu katika kuisaidia jamii.

Aidha, alitoa shukrani kwa ujenzi wa Misikiti na Madrasa katika maeneo mbalimbali hapa nchini, na kusema hatua inasaidia uendelezaji wa Dini ya Kiislamu.

Rais Dkt.Mwinyi alisema Serikali itatoa msukumo ili kufanikisha ujenzi wa Barabara ya Birikau Kisiwani Pemba pamoja na kuuagiza Uongozi Kikosi cha Kuzuia Magendo KMKM kutoa elimu kwa wamiliki wa boti za kusafirishia wananchi katika maeneo ya Visiwa kisiwani Pemba ili kuwahakikishia usalama katika safari za baharini.

Mapema, Mkuu wa Miradi wa Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, Khadija Ahmeid Sharrif alisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia jamii kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya uimarishaji wa afya, elimu, maji pamoja na uwezeshaji ujasiriamali.

Alisema, taasisi hiyo imekuwa ikisaidia uimarishaji wa afya ya mama na mtoto kwa kuendeleza ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba, kusaidia vifaa vya tiba pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta hiyo.

Aidha, alisema taasisi hiyo inatoa msukumo mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini kwa kufanikisha ujenzi wa majengo ya skuli pamoja na kutoa kusaidia upatikanaji wa mbinu sahihi za kufundishia pamoja na kufanya tafiiti.

Vile vile alisema, taasisi imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wajasiriamali, wakiwemo akinamama na vijana katika kustawisha kilimo cha zao mwani pamoja na kulifanyia usarifu wa zao hilo ili kuwaongezea kipato.

Naye Meneja wa Taasisi ya IFRAJ, Abdalla Said Abdalla alisema taasisi hiyo imekuwa ikijishughulisha na ujenzi wa nyumba za makazi kwa wananachi wenye kipato cha chini, ambapo hvii sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 500 zinazogharimu zaidi ya shilingi bilioni 7.5.

Aidha, alisema taasisi hiyo pia imekuwa ikijishughulisha na ujenzi wa nyumba za ibada ikiwemo Misikiti na Madrasa katika maeneo mbalimbali nchini, kusaidia wajene na yatima pamoja na kutoa chakula kwa wanafunzi.
Vile vile imekuwa ikisadia ujenzi wa kliniki,majengo ya skuli, kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kwa kuchimba visima na kusaidia upatikanaji wa pampu pamoja na kusaidia huduma muhimu wakati wa majanga ikiwemo matukio ya moto.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Taasisi ya Zanzibar Milele Foundation mara baada ya mazungumzo yao leo Ikulu jijini Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Ahmeid aliomba Serikali kusaidia wataalamu watakaoweza kutoa elimu kwa wamiliki wa boti za kusafirishia wananchi kwenye Visiwa ili kuepusha ajali, huku akibainisha azma ya taasisi hiyo kusaidia upatikanaji wa mavazi ya uokozi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news