Rais Dkt.Mwinyi:Uzazi ni uhai,tuwajibike wote kuepusha vifo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, kupungua na kuepusha vifo vya akinamama na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi hapa nchini, ni jukumu linalohitaji ushiriki wa kila mtu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiongoza matembezi ya kilomita tano yaliyofayika leo kuanzia viwanja wa Maisara Suleiman jijini Zanzibar hadi uwanja wa Amaan Studium ikiwa ni kampeni ya “Uzazi ni Maisha”yaliyoandaliwa na Jumuiya ya AMREF HEALTH AFRICA ,ambapo viongozi mbalimbali wameshiriki katika matembezi hayo. (Picha na Ikulu).Dkt.Mwinyi amesema hayo katika Uwanja wa Amani uliopo Mjini Magharibi baada ya kukamilika kwa zoezi la mbio fupi na matembezi ya hiari, ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya Uzazi ni Maisha.

Amesema, kuna umuhimu kwa kwa kila mtu mahali alipo, ikiwemo sekta binafsi, mashirika na asasi zisizo za kiserikali kushiriki kikamilifu katika kupunguza na kuepusha vifo vya akinamama na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi.

Mheshimiwa Rais amesema, ili kufikia lengo hilo kuna umuhimu wa kuwaaminisha akinamama waja wazito kwamba uzazi ni uhai ili waamini kuwa lengo la uzazi ni kuleta maisha mapya duniani na sio kuondoa maisha ya wazazi.

Amesema kuwepo, kwa idadi kubwa ya vifo vya akinamama hapa nchini vitokanavyo na uzazi kunachangiwa na changamoto mbalimbali , ikiwemo ile iliyopo katika mifumo ya utoaji huduma za afya, upungufu wa vifaa tiba na dawa, ufinyu wa miundombinu, uchache wa madaktari na wauguzi na baadhi ya wakati suala la mila na utamaduni.

Dkt. Mwinyi ambaye aliambatana na mkewe Mama Mariamu Mwinyi alitumia fursa hiyo kubainisha takwimu za matukio ya vifo vya wazazi hapa nchini vitokanavyo na uzazi kuwa vimefikia vifo 134 kwa kila wajawazito 100,000 na watoto 37 kwa kila vizazi 1,000.

Alisema hatua ya Serikali kujenga Hospitali za Wilaya pamoja na Hospitali ya Mkoa Mjini Magharibi unalenga kuondoa msongamano wa wananchi wanaofuata huduma katika Hospitali ya Mnazimmoja na Abdalla Mzee Mkoani Pemba ili kupunguza vifo.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wanamichezo walioshiriki zoezi hilo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya, utoaji wa mafunzo pamoja na kutekeleza mpango uliopo wa kuanzisha Bima ya Afya, sambamba na kuongeza Bajeti ya Wizara ay Afya.

Dkt. Mwinyi alisema amefurahishwa na taarifa kuwa jumla ya vituo 28 vitaweza kupata vifaa tiba kati ya vituo 70 vinavyotoa huduma ya mama na mtoto Unguja na Pemba.

‘Kwa kutambua juhudi hizo Serikali nayo itahakikisha inafanikisha upatikanaji wa vifaa tiba kwa asilimia 60 ya vituo iliyobaki,”amesema.

Alieleza kuwa juhudi za kumarisha huduma za mama na mtoto zinapaswa kwenda sambamba na hatua ya utoaji wa elimu kwa makundi mbali mbali ndani ya jamii.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza waandaaji wa Kampeni hiyo AMREF Health Africa, pamoja na wadhamini mbalimbali waliofanikisha shughuli hiyo, ikiwemo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Nae, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui alisema ujio wa kampeni hiyo unathibitisha kwa kiasi gani Serikali ilivyojidhatiti kushughulikia suala la Afya ya mama na mtoto hapa nchini.

Aidha, ,Mkurugenzi Mkazi wa AMREF Health Africa,Dkt.Florence Temu katika salamu zake alisema AMREF kwa kushirikiana na Wizara Afya imekuja na Kampeni hiyo kwa lengo la kuhamasisha upatianaji wa vifaa tiba kama nyenzo ya kutatua changamoto za uzazi salama, kuongeza uwelewa na hamasa kwa jamii pamoja na ushirikishwaji,

Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC Theobaid Sabi alisema benki hiyo ni muumini mkubwa wa falsafa ya kusaidia jamii, akiabainisha kila mwaka hutenga fedha kwa ajili ya kusaidia jamii katika maeneo mbali mbali, ikiwemo Afya, elimu, uwezeshaji na mengineyo.

Kampeni ya ‘Uzazi ni maisha’ iliobeba ujumbe wa ‘Changia vifaa tiba kwa uzazi salama’, iliwashirikisha wanamichezo na vikundi mbali mbali vya mazoezi hapa Zanzibar, ambapo ilianzia Maisara na kumalizikia Uwanja wa Amani.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmeid Said pamojana viongozi mbalimbali wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news