Rais Dkt.Mwinyi apokea ripoti ya CAG, atoa onyo kali

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kujitathmini juu ya utendaji wake, kutokana na kuwepo kwa matukio kadhaa ya wizi wa mali za Serikali na uhujumu uchumi ambapo taasisi hiyo imeshindwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Dkt.Mwinyi ametoa wito huo Ikulu jijini Zanzibar, baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia mwezi Juni 30, 2021.

Amesema, ni muhimu kwa taasisi hiyo kujitathimini juu ya utendaji wake wa kazi, kwa kigezo kuwa kumekuwepo kesi nyingi za wizi wa mali za Serikali na uhujumu uchumi, ambapo mbali na kukabidhiwa kuzishughulikia lakini hakuna mrejesho kwa kipindi kirefu sasa.

Amesema kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya kesi hizo watuhumiwa wamekiri kuhusika na matukio hayo na wengine kukubali kurejesha fedha serikalini, lakini hakuna hatua za kisheria zilizobainishwa kuchukuliwa.

Dkt.Mwinyi alitolea mfano wa tukio la wizi wa fedha lilitokea ZRB kupitia mfumo wa Mtandao, ambalo hadi sasa halijaainishwa hatua zilizochukuliwa na kusema utamaduni huo umefanya vitendo kama hivyo kujirejea mara kwa mara.

“...bado hawajaisaidia serikali kumekuwa na matukio kadhaa kuripotiwa ndani ya kipindi cha miaka miwili sasa,"amesema.

Dkt.Mwinyi ameagiza hatua thabiti zichukuliwe dhidi ya watu wote watakaohusishwa na matukio ya wizi wa fedha za umma, na kusema kamwe nchi haiwezi kuendelea kwa namna hiyo ikiwa kila mahali kuna matukio ya wizi.

Amewataka viongozi wote walioko serikalini kuona ukubwa wa tatizo hilo na kutaka hatua za msingi kuchukuliwa kwa wote waliohusika.

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali ilifanya uamuzi wa kuondoa jukumu la Wizara ya Afya kununua dawa na jukumu hilo kulikabidhi Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, lakini inashangaza uongozi wa Hospitali hiyo nao unanunua dawa hizo kwa wauzaji wale wale waliokuwa wakichangia upotevu wa fedha nyingi za Serikali.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza kwa dhati CAG, Dkt.Othman Abass Ali kwa moyo wa kujitolea na kubainisha kasoro mbalimbali zilizopo katika wizara na taasisi za Serikali.

“Laiti kama kazi inayofanywa na CAG ingefanywa na vyombo vingine vinavyohusika, matukio kama haya yasingejirudia,”amesema.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali imepokea taarifa hiyo na ushauri wenye nia ya kupunguza au kuondoa kabisa matatizo hayo, hivyo akatumia fursa hiyo kumtaka Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmeid Said kuwafikishia watendaji wote wa wizara na taasisi za serikali mapendekezo yaliyotolewa na CAG.

Mapema, akiwasilisha taarifa ya ukaguzi, Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Dkt.Othman Abass alitoa mapendekezo mbalimbali, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na wimbi la wizi wa fedha za Serikali pamoja na kasoro zinazopelekea kusababisha upotevu wa fedha za Serikali.

Amesema, kuna umuhimu kwa Serikali kuanzisha mfumo wa uwekaji zabuni ili kuepuka madeni feki, pamoja na kuishauri Serikali kuvunja mikataba yote ya Ununuzi na Usambazaji wa Dawa na Vifaa tiba inayotumiwa na Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili kuokoa fedha nyingi za Serikali zinazoendelea kupotea.

Ameishauri Serikali kuanzisha mfumo mpya wa upokeaji dawa na usambazaji wake ili kuepuka kupokea dawa zilizopitwa na muda na zisizofaa kwa matumizi ya afya ya binadamu, jambo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara.

Aidha, Dkt.Abass ameshauri taasisi zote za Serikali zinazotekeleza miradi ya maendeleo kufanya upembuzi yakinifu ili kuhakikisha thamani ya fedha inayotumika kufanikisha miradi hiyo inaendana na kazi inayofanyika.

Katika ripoti hiyo, Dkt.Abass aliwasilisha matukio mbalimbali yaliyojiri katika kipindi hicho, huku akibainisha mabilioni ya Fedha za Serikali zilivyoibiwa au kupotea kutokana na kasoro za kiutendaji.

Miongoni mwa wizara ilioelekezwa shutuma nzito ya wizi wa fedha hizo ilikuwa ni Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 zimeibiwa baada ya kutolewa katika Akaunti ya Wizara na kuelekezwa katika akaunti za kampuni mbalimbali bila kazi yoyote kufanyika.

Aidha, aeneo jingine ambalo limenyooshewa kidole kujiri kwa upotevu mkubwa wa fedha za Serikali ilikuwa ni Mashirika ya Umma , ikiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) uliohusishwa na hatari ya kufilisika kutokana na mwenendo mbaya wa urudishaji mikopo katika maeneo tofauti, ikiwemo ujenzi wa majengo, uendeshaji wa miradi kadhaa isiyoleta tija, kama vile uwekezaji katika Hoteli Pemba pamoja na kuwakopesha wafanyakazi wake bila kuzingatia kanuni.

Vile vile Shirika la Bandari nalo likahusishwa na upotevu wa fedha nyingi za Serikali, ambapo pamoja na kasoro mbalimbali zilizobainika, limehusishwa na upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 732 kwa kushindwa kukusanya mapato kutokana na uwekaji wa bidhaa, ambapo pale wafanyabiashara wanaposhindwa kutoa bidhaa zao bandarini, huzunguka na kuzinunua bidhaa hizo kwa kiwango kidogo cha fedha pale zinaponadiwa kwa na hivyo kuipotezea serikali mapato.

Idara ya pensheni jamii nayo ni miongoni mwa zilizobainika kuwa na kasoro na upotevu mkubwa wa fedha, kutokana na kushindwa kurejesha Hazina bakaa ya fedha, kuwepo matumizi hewa ya takriban shilingi milioni 75 huku kukiwa hakuna wazee waliolipwa.

Akigusia juu ya Uhakiki wa Mafao ya Viinua Mgongo na Pensheni kwa wastaafu wa Serikali na Mashirika ya umma, Dkt.Abass amesema, eneo hilo lina changamoto nyingi, ikiwemo ya kutokuwepo kwa taarifa sahihi za wastaafu pamoja na baadhi ya wastaafu, hususani kutoka vikosi vya SMZ kuendelea kulipwa mishahara hata baada kustaafu kazi.

Dkt.Abass aliiitaja Wizara ya Afya kuhusika na uwasilishaji wa madeni feki katika uhakiki wa Zabuni za Madawa na Vifaa Tiba.

Amesema, kuna matukio kadhaa kwa wizara hiyo kuwasilisha kwake madeni ya kiwango cha juu cha zabuni, lakini pale yanapohakikiwa hubainika kiwango halisi kuwa cha hali ya chini.

Alitolea mfano wa deni la zabuni ya shilingi bilioni 4.922 lililowasilishwa kwake, lakini baada ya kufanya uhakiki ikabainika kuwa deni halali ilikuwa ni shilingi milioni 886.68.

“Kuwepo kwa deni danganyifu lililoripotiwa Wizara ya Afya, tulimtaka Mkurugenzi wa Bohari athibitishe kwa maadishi...baada ya wiki tulisikia amekufa,”amesema.

Mapema, CAG alitoa taarifa kuhusiana na Gawio la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi kufuatilia gawio hilo ili kupata ufumbuzi.

Amesema amebaini kiasi cha shilingi Bilioni 4.8 hazijapokelewa na serikali kutokana na gawio hilo ambapo SMZ ilipaswa kupokea shilingi Bilioni 57.6, wakati ambapo fedha zilizotoka ni shilingi Bilioni 52.8.

Akigusia juu ya usimamizi wa Fedha za Muungano kupitia Akaunti ya pamoja ya fedha, Dkt.Abass amebainisha kutokuwepo kwa maoni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yangepaswa kuwasilishwa ili yafanyiwe kazi na SMT, hivyo hatua hiyo imemfanya ashindwe kubaini kiwango halisi cha fedha kilichotumika kufungua akauni hiyo.

Katika taarifa hiyo, Dkt.Abass alibainisha kasoro kadhaa za kiutendaji zilizobainika pamoja na kiwango kikubwa cha upotevu wa fedha katika wizara na taasisi za Serikali pamoja na Vikosi vya SMZ ikiwemo JKU, Mafunzo, KMKM, Zimamoto pamoja na Kikosi cha Valantia.

Aidha, aliorodhesha miradi kadhaa ya maendeleo iliyobanika kuwa na dosari, ikiwemo kufanya matumizi ya ziada ya fedha zilizotengwa katika bajeti, ununuzi hewa wa vifaa pamoja na baadhi ya taasisi kushindwa kuwalipa fidia wananachi, mbali na fedha za kazi hiyo kutengwa.

Akitoa mfano aliutaja Mradi wa kudhibiti VVU, akisema mradi huo ulipangiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 48.2 kwa ajili ya ununuzi wa dawa aina ya Methadone, lakini katika ukaguzi aliofanya hakubaini taarifa yoyote ya kupokelewa kwa dawa hizo, mbali na fedha hizo kulipwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news