Rais Samia aagiza Kituo cha Malezi ya Watoto kijengwe Soko Kuu Njombe Mji

NA OR-TAMISEMI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan ameagiza kituo cha malezi ya watoto kijengwe katika Soko Kuu la Njombe Mji ili kina mama wanapoendelea na shughuli zao za biashara watoto wao wapate sehemu ya kujifunza na kupumzika.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Agosti 10, 2022 wakati akifungua Soko Kuu la Njombe Mji na kuridhishwa na miundombinu ya soko hilo na utaratibu uliowekwa wa kuwapanga wafanyabiashara wa soko hilo.

"Wafanyabiashara hawa sasa ni rasmi, hapo awali walikuwa wanafanya biashara kwenye maeneo ambayo si rasmi na wengine kwenye miundombinu chakavu nimeona picha ya soko la zamani, lakini kwa hapa sasa walipo kwa kweli panavutia.

"Pamoja na kuona wafanyabiashara wakiwa katika mazingira bora, lakini nimeona akina mama wakiwa wamebeba watoto mgongoni sasa niwaagize Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Mkurugenzi kuangalia namna ya kutenga eneo na kujenga Kituo cha Malezi ya Watoto ili mama zao wanapoendelea kufanya biashara watoto waweze kujifunza a,b,c.

“Lakini na akina mama muwe tayari kuchangia kidogo ili wale walezi wanaokaa na watoto wenu na kuwafundisha waweze kupata chochote, kwa hiyo hili mkoa mliangalie na mlifanyie kazi,"amesisitiza Mhe.Rais Samia.

Soko kuu la Kisasa la Njombe Mji lina ukubwa wa mita za mraba 9,186, sakafu (floors) tatu, lina mifumo na sehemu mbalimbali yakiwemo maduka 162, meza za biashara 407, vyoo 47, migahawa miwili, stoo sita, vizimba vya kuku 27, machinjio ya wanyama wadogo, sehemu za huduma za kibenki mbili, ofisi za utawala mbili, mfumo wa maji safi na maji taka na kisima kirefu cha maji.

Pia soko hilo lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 680 na limegharimu shilingi bilioni 10.2 hadi kukamilika kwake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news