Mabalozi wa Tanzania wafunguka kuhusu fursa za kiuchumi Ulaya

NA DIRAMAKINI

IMEELEZWA kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake wana nafasi kubwa ya kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo nchi za Bara la Ulaya kunufaika kiuchumi, kutokana na misingi mizuri ya uimarishaji wa diplomasia ya uchumi iliyowekwa na Serikali.
Hayo yamesemwa kwa nyakati toafauti leo Agosti 10, 2022 na watoa mada ambao ni wanadiplomasia wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mataifa mbalimbali barani Ulaya.

Ni kupitia mkutano muhimu na maalum ulioratibiwa na Watch Tanzania kupitia Mtandao wa Zoom ambapo umeangazia juu ya KUKUA KWA DIPLOMASIA YA UCHUMI NA FURSA ZA KIUCHUMI ZINAZOPATIKANA NCHI ZA BARA LA ULAYA. Washiriki wa mkutano huo wamesema;

BALOZI MHE. ASHA-ROSE MIGIRO BALOZI WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA

"Uingereza imekuwa mshirika mkubwa sana wa maendeleo katika nchi ya Tanzania, kwani imeweza kusaidia na kushirikiana na Serikali yetu katika utimilifu wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya ujenzi, sekta ya kilimo na ufugaji na hata Sayansi na Teknolojia;
"Tanzania sasa hivi hatufanyi biashara na Uingereza kama mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya, lakini kama nchi inayosimama pekee yake, lakini utaratibu ni ule ule kama Jumuiya ya Ulaya, kwani wamerahisisha kanuni zake za biashara kwa kuweka masharti rahisi,"amesema Balozi Asha-Rose Migiro.

BALOZI MHE.GRACE ALFRED OLOTU, BALOZI WA TANZANIA NCHINI SWEDEN

"Sweden ina miradi nchini Tanzania isiyopungua 200 kutoka makapuni mbalimbali, miradi hiyo ina thamani ya dola za Kimarekani milioni 726.63 na inachangia ajira za moja kwa moja zipatazo 15,191;
"Kwa hiki kipindi cha muda mfupi tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani nchi yetu imeweza kujitangaza zaidi na kumeonekana kuwa na fursa nyingi sana za uwekezaji, hivyo wafanyabiashara wengi wametamni kuja kufanya uwekezaji mbalimbali, hivyo vikao vinaendelea kuimarisha zaidi mahusiano hayo baina ya hizi nchi zetu,"amesema Balozi Olotu.

BALOZI JESTUS NYAMANGA, BALOZI WA TANZANIA NCHINI UBELIGIJI

"Moja ya faida ya kibiashara ambayo Watanzania wanaweza kunufaika nayo ni kwamba nchi yetu Tanzania inauza sana bidhaa nchini Ubeligiji kuliko tunavyonunua, kwani mwaka jana tuliuza bidhaa za Euro millioni 75.2 na wao waliuza bidhaa za Euro milioni 72.5;
"Mwaka huu wa 2022 umekuwa ni mwaka wa neema sana, kwani tangu mwezi Januari mpaka Aprili tumeuza nyinging, inaonesha miezi minne tu tumeuza bidhaa za mwaka mzima, hii ni hatua kubwa sana,"amesema Balozi Nyamanga.

BALOZI MHE. SAMWEL SHELUKINDO, BALOZI WA TANZANIA NCHINI UFARANSA

"Ndani ya hii miaka miwilii Shirika la Maendeleo la Ufaransa limeweza kuongeza misaada zaidi kwa masharti nafuu kutoka Euro milioni 100 kwa mwaka kufikia milioni 150;
"Mikataba Rais Samia Suluhu Hassan aliyosaini huku UFaransa ni pamoja na ;

1. Miradi ya kimkakati (SGR, JNHS n.k)

2. Uchumi wa bluu Zanzibar na Usalama wa bahari kuu

3. Usafirishaji wa mizigo

4. Ujenzi wa kiwanja cha ndege Terminal 2 ,"amesema Balozi Shelukindo.

BALOZI MHE.MAIMUNA TARISHI BALOZI MWAKILISHI WA KUDUMU UMOJA WA MATAIFA (UN), GENEVA, USWISI

"Kupitia ziara mbalimbali za viongozi wetu wameweza kushiriki mikutano mbalimbali ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na kupata fursa mbalimbali ikiwemo kupokea dola za kimarekani takribani milioni 3.5 ambazo ni sawa na bilioni 7 za kitanzania, ambazo sio mkopo zilitolewa na Shirika la Biashara Duniani (WTO) kwa ajili ya kuongeza thamani za mbogamboga na matunda nchini;
"Chini ya mpango wa WTO, Shirika la Biashara Duniani wataweza kusimamia upatikani wa masoko ya mazao ndani na nje ya nchi, mafunzo kwa taasisi mbalimbali ikiwemo SIDO, wametoa magari matatu ambayo mawili yanatumika Tanzania Bara na moja visiwani Zanzibar,"amesema Balozi Tarishi.

BALOZI DKT.ABDALLAH POSSI BALOZI WA TANZANIA NCHINI UJERUMANI

"Utalii ni moja ya fursa kubwa sana kwa nchi ya Ujerumani kuja Tanzania, kwani kutokana na kipindi cha Low na High Session tunategemea 2023 watalii watakuja zaidi ya 90,000 kwa mwaka;
"Ujerumani wana uhaba wa mbogamboga na matunda, hivyo pongezi nyingi ziende kwa Taasisi ya TAA ambayo imekuwa ikionesha maonesho ya bidhaa mbalimbali ambazo hufanya uhitaji wake kuwa mkubwa nchini Ujerumani,"amesema Balozi Possi.


BALOZI YACOUB MOHAMMED, BALOZI WA TANZANIA NCHINI UTURUKI

"Ziara ya Mhe.Rais wa Uturuki Tayyip Erdoğan mwaka 2017 nchini Tanzania iliibua masuala mengi pamoja na kufunguliwa ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki na kuzidi kuimarisha diplomasia kwa nchi zote mbili;
"Kumekuwa na bidhaa nyingi toka Uturuki zikitumika Tanzania, hivyo kama balozi tunajitahidi kuwashawishi wamiliki wa viwanda kufungua viwanda hivyo nchini, ili bidhaa hizo zipatikane kwa urahisi, kwa bei nafuu, kutumia mali ghafi zetu na hivyo kuongeza soko la ajira kwa vijana wa Tanzania,"amesema Balozi Luteni Jenerali Mohamed.

BALOZI CELESTINE J. MUSHI BALOZI WA TANZANIA NCHINI AUSTRIA

"Diaspora ya hapa nchini imenisaidia sana kujua uongozi na viongozi wa hapa na kujadili ni kwa namna gani tunaweza kukuza uhusiano wetu na nchi ya Austria na kuchangamkia fursa zilizopo, kwani Ubalozi wetu bado ni mchanga.

"Kutangaza fursa zinazopatikana nchini Austria moja ya nyenzo ni kutumia Watanzania walioishi hapa nchi hii kwa muda mrefu (Diaspora), hivyo nilivyofika nilianza kuandikisha Watanzania waishio Austria na idadi yake kuwa 118," amesema Balozi Mushi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news