Rais Samia awapongeza Wakenya kwa uchaguzi wa amani, utulivu

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Jamhuri ya Kenya kwa kushiriki uchaguzi wao mkuu kwa amani na utulivu.

Pongezi hizo zinakuja ikiwa Jamhuri ya Kenya imefanya uchaguzi wa saba tangu nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki kuanza mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ikiwa ni miaka 30 iliyopita.

Uchaguzi wa Agosti 9, 2022 ulikuwa ni wa tatu tangu kupatikana kwa katiba mpya mwaka 2010 ambapo Rais Uhuru Kenyatta anamaliza muda wake kwa sasa.
Mheshimiwa Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Agosti 16, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kutangaza matokeo ya urais kwa maana ya Agosti 15, 2022.

"Ninapenda kuwapongeza kwa dhati wananchi wa Kenya kwa kushiriki uchaguzi wao mkuu kwa amani na utulivu, ambapo matokeo yake ni Dkt.William Ruto kutangazwa kuwa Rais mteule wa Kenya. Tanzania itaendeleza undugu na ushirikiano wa kihistoria na Kenya uliodumu miaka na miaka,"ameeleza Mheshimiwa Rais Samia.

Katika uchaguzi huo, ushindani mkubwa ulikuwa kati ya Naibu Rais, Dkt.William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga.

Dkt.Ruto na Odinga waliwahi kuwa katika chama kimoja cha KANU wakati wa utawala wa aliyekuwa hayati rais wa Kenya, Daniel Arap Moi na pia ni ndio waanzilishi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Jana Mwenyekiti wa IEBC,Bw.Wafula Chebukati alimtangaza Dkt.Ruto kwa kushinda uchaguzi huo kwa kupata kura milioni 7.18 sawa na asilimia 50.49, huku mpinzani wake wa karibu, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga akipata kura milioni 6.94 sawa na asilimia 48.85.

“Nasimama mbele yenu kutangaza matokeo haya, licha ya kutishwa sana, nimefanya jukumu langu la kikatiba.Kwa mujibu wa Katiba, namtangaza William Ruto kuwa rais mteule,”alisema Chebukati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news