Serikali yaweka mezani Bilioni 570/-mikopo elimu ya juu nchini

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imetenga zaidi ya shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi ambao wanakidhi vigezo elimu ya juu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari juu ya Mwelekeo wa Wizara, Vipaumbele na Maeneo ya Kimkakati katika Utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

"La kwanza ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu mikopo ya elimu ya juu kwa ujumla wake kwa sababu inasaidia upatikanaji wa elimu,tumetenga shilingi bilioni 570 kwa ajili ya upatikanaji wa elimu ya juu na tayari tumeshafungua dirisha la uombaji wa mikopo.

"Narudia tena kusisitiza watu wajaribu kufuata taratibu sasa hivi tunafanya audit (ukaguzi) kwa taratibu za utoaji wa mikopo kuhakikisha kwamba imetolewa kwa haki," amesema Prof.Mkenda.

Mheshimiwa Waziri amefafanua kuwa, "Tunaangalia kinachofanyika. Mimi binafsi nimeridhika, lakini tunasema trust but verify kwa hiyo tumeunda timu ya watu watatu kutoka Zanzibar na Bara wanapitia mikopo imekuwa ikitolewa vipi na nani amekuwa akiipata.

"Kwa sababu kuna watu wamekuwa wakikosa mikopo kwa sababu ya kutotoa taarifa ama ambazo ni muhimu na ushahidi unaotakiwa,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Prof.Mkenda.

Wanaoongoza tume

Amesema tume hiyo itaongozwa na Prof. Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya Kompyuta na Takwimu.

Waziri Prof.Mkenda amesema, tume hiyo itachunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo kwa watu wasiokuwa na sifa.

Amesema kuwa, tume hiyo itapitia malalamiko ya wanafunzi mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji mikopo kwa kupata mikopo kwa wanafunzi wenye sifa huku wale wasiokuwa na sifa stahiki wakikosa mikopo hiyo.

“Na kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma nae utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa.

“Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo tunamkaribisha ili aweze kuisaidia tume kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa hali ya juu kutoka kwa wanachi husika,”amefafanua.

Prof.Mkenda amesema kuwa, tume hiyo itaangalia vigezo vilivyoainishwa ili kuona kama kuna taarifa zingine za ziada zinaweza kutumika katika utoaji wa mikopo ili fedha zinazotolewa na serikali zikopeshwe kwa haki.

Ufaulu mzuri

Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri Prof.Mkenda amesema,"kwa mara ya kwanza tangu tumeanza tutakuwa na shilingi bilioni 3 zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi waliofanya vizuri sana mitihani kupitia Baraza la Mitihani la Taifa kupitia masomo ya Sayansi ambao watachagua kuendelea na masomo ya Sayansi, uhandisi na masomo ya elimu tiba.

"Vigezo viko viwili cha kwanza, uwe umefaulu vizuri sana katika masomo ya sayansi, halafu pili upo tayari uendelee tena kusoma masomo kwenye masomo ya sayansi, na masomo ya elimu tiba.

"Humo tutachagua ambao ni wajuu kabisa kwa hizo shilingi bilioni tatu watasomeshwa na Serikali mpaka watamaliza na hii kila mtu anasema iitwe Samia Scholarship kwa sababu imeanza kipindi cha Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Na hii haitajalisha unatoka familia maskini au tajiri kwa sababu tunataka kuwekeza kwenye ubongo ambao unaonekana unachangia sana katika maendeleo ya nchi yetu.

"Kwenye maeneo ya Sayansi na teknolojia na hilo liko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hii ni aina ya utekelezaji wake, kwa sasa hivi hizi Scholarship zitatumika kwenye vyuo vyetu vya ndani tu.

"Lakini huko tunakokwenda tutajitahidi kupeleka kwenda kusoma katika vyuo vya nje na kadhalika, hiyo ni sehemu mojawapo ya kuhakikisha kwamba kuna upatikanaji wa elimu, lakini kutoa kama kivutio kwa wanafunzi wanaofanya vizuri sana kwa mfano PCM, wengine wanaacha kusoma masomo ya sayansi wanataka kwenda kusoma masomo ya biashara kwa sababu wanaona labda kuna fursa kubwa, lakini nchi haiwezi ikaendelea bila kuwekeza katika masomo ya sayansi na teknolojia na elimu tiba.

"Vile vile pamoja na hiyo mtakumbuka Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha na Mipango ametangaza kutenga Shilingi Bilioni 8 kupitia mfumo wa TASAF kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kusoma.

"Pia tumeongea na Benki ya NMB ambayo nayo imetenga Shilingi Bilioni 200 sasa hizi Bilioni 200 zitatolewa kama mkopo na tumeweza kupata riba ndogo asilimia 9 kwa wale ambao wanapitisha mapato yao kupitia NMB akitaka kwenda kusoma chuo cha Ufundi VETA na kadhalika unaweza ukachukua mkopo dhidi ya kile ambacho unakipata kinapitia NMB.

"Mkopo huu wa shilingi Bilioni 200 utawanufaisha wale ambao pengine wanalipwa mshahara unapitia NMB halafu kwa makubaliano hayo utapata mkopo,"amesema Prof. Mkenda.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Profesa Mkenda amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuwekeza zaidi katika elimu, sayansi na teknolojia kwa manufaa ya Taifa na jamii.

"Najua elimu, sayansi na teknolojia ni mambo muhimu sana kwa nchi zote duniani ukiangalia kwa nchi ambazo zimeendelea kigezo kikubwa cha maendeleo yao ni uwekezaji wao katika elimu, masuala ya elimu katika sayansi na teknolojia siyo ukubwa wa nchi.

"Hata ukiangalia nchi ambazo zimepiga hatua kubwa hazipigi hatua eti kwa sababu zina populations kubwa ila kwa sababu zimewekeza sana katika elimu, kwa hiyo tunaweza tukaunganisha East Africa Community tukajenga soko kubwa bila elimu tukajikuta tuna changamoto.

"After all, Singapore ni nchi ndogo kijografia ila imepiga hatua kubwa sana wakati tunajitahidi kupanua soko la Afrika Mashariki tunahitaji kuwekeza katika elimu na vile vile nchi haziendelei kwa sababu ya rasilimali za asili si madini wala mafuta ni kwa sababu ya kuwekeza katika elimu.

"Kwa hiyo kupitia elimu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo nini kifanyike katika elimu na ni wajibu wetu sisi kuwaeleza umma na ni hatua gani zinazochukuliwa.

"Ili waelewe kwamba kweli Serikali imejipanga kwa ajili ya kukidhi kiu yao ikiwemo kuongeza ubora wa elimu na kuhakikisha kwamba inapatikana kama inavyotakiwa.

"Hapa nitazungumzia mambo makubwa mawili ya kimkakati ambayo tuliyazungunza wakati wa bajeti na jinsi ambavyo tunayatekeleza.

"Lakini kabla ya kuzungumza nataka tu nifafanue katika elimu kuna vitu viwili vikubwa, mosi kuna ubora wa elimu, na upatikanaji wa elimu yenyewe. Unaweza ukawa na elimu bora, lakini upatikanaji wa elimu hiyo ni kwa wachache sana.

"Watu wanataka ubora wa elimu na upatikanaji wake,so we want quality and access to education na kwenye quality education of course ni uelewa wa jinsi ambavyo unahakisi mahitaji yako ya pale na unapoishi na dunia inavyokwenda.

"Nitaanza kidogo na upatikanaji wa elimu hatua ambazo Serikali inazichukua na mnazofahamu zote kupitia kwanza kwenye bajeti yetu ambayo ni takribani shilingi trilioni 1.49 kwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na hapa hatujachanganya na wenzetu wa TAMISEMI (Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ambapo pia wanatusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya elimu,"amefafanua Prof.Mkenda.

Hata hivyo,dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 lipo wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30, mwaka huu.

Waziri Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2022/2023 ili kuwasilisha maombi kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi zilizowekwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news