TET yataja sababu za mapitio makubwa ya mitaala ya elimu

NA MWANDISHI WETU

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imesema tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, imefanya mapitio makubwa sita ya mitaala ya elimu lengo likiwa ni kuwajengea wahitimu ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kutumia vema fursa zinazopatikana nchini, husani kwa kujiajiri, kuajiriwa na kumudu maisha yao ya kila siku pale wanapohitimu mafunzo.
Kati ya mapitio hayo, matano tayari yalishafanyika mpaka kufikia mwaka 2014, na sasa kazi ya kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya pitio la sita inaendelea.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt.Aneth Komba amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa shughuli za Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na mwelekeo wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

“Mapitio ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 kwa lengo la kuondoa mitaala ya kibaguzi ya wakoloni, mapitio ya pili yakafanyika mwaka 1979 kwa lengo la kuhimiza matumizi ya nadharia, na kupitia mapitio hayo kulianzishwa masomo ya michepuo, mapitio ya tatu yakafanyika mwaka 1997 ambayo lengo lake lilikuwa kukidhi matakwa ya sera ya mwaka 1995 pamoja na kuingiza mapendekezo ya Tume ya Makweta ya mwaka 1982.

"Mapitio ya nne yalifanyika mwaka 2005 ambayo yalipelekea kuanzishwa kwa mtaala ambao ulilenga kujenga umahiri, na mapitio ya tano yalifanyika mwaka 2014 ambayo yalikuwa na lengo la kuingiza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia elimu ya awali,”amesema Dkt.Komba.

Aidha, ameeleza kuwa katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilitoa Fedha jumla ya Shilingi Bilioni 1.4 ambazo zimetumika kukusanya maoni ya wadau, kuchakata taarifa na kuandaa rasimu za mitaala ya ngazi zinazopendekezwa.

‘’Katika kukusanya maoni jumla ya wadau 103,210 wamefikiwa, awali, TET ilipokea maoni ya wadau kupitia mikutano mikubwa mitatu iliyofanyika jijini Dar es salaam, Dodoma na Zanzibar, aidha TET ilikusanya maoni kupitia vikao vilivyofanywa na makundi mbalimbali.

"Pia maoni mengine yalipokelewa kwa kutumia namba ya simu, barua pepe, sanduku la barua, kiunganishi kwenye tovuti ya TET, dodoso na hojaji,”amesema Dkt.Aneth Komba.

Akizungumzia Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, Dkt. Komba amesema TET imejipanga kuwashirikisha wadau kuhusu rasimu za mitaala zilizopendekezwa, na kuendelea na hatua ya kuandaa vifaa vingine vya utekelezaji wa mitaala ikiwemo mihtasari pamoja na kutoa mafunzo ya walimu na wasimamizi wengine wa utekelezaji wa mitaala.

‘’Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya shilingi 1,769,340,000 kwa kazi hii inayotarajiwa kukamilika Disemba, 2022. Naomba nisisitize kuwa katika kufanya kazi ya mapitio ya mitaala zoezi la kukusanya maoni kutoka kwa wadau ni endelevu,’’amesema Dkt.Aneth Komba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news