TUSIBAKI HALI HII: Wizi na kuzungushana, kukome na kukatika, Rais Dkt.Mwinyi hatanii

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

AGOSTI 27, 2022 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kujitathmini juu ya utendaji wake, kutokana na kuwepo kwa matukio kadhaa ya wizi wa mali za Serikali na uhujumu uchumi ambapo taasisi hiyo imeshindwa kuchukuwa hatua za kisheria.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikisomwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dkt. Othman Abass Ali (kushoto kwa Rais) kabla ya kumkabidhi,hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.

Dkt.Mwinyi ametoa wito huo Ikulu jijini Zanzibar, baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia mwezi Juni 30, 2021.

Amesema, ni muhimu kwa taasisi hiyo kujitathimini juu ya utendaji wake wa kazi, kwa kigezo kuwa kumekuwepo kesi nyingi za wizi wa mali za Serikali na uhujumu uchumi, ambapo mbali na kukabidhiwa kuzishughulikia lakini hakuna mrejesho kwa kipindi kirefu sasa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya kesi hizo watuhumiwa wamekiri kuhusika na matukio hayo na wengine kukubali kurejesha fedha serikalini, lakini hakuna hatua za kisheria zilizobainishwa kuchukuliwa.

Dkt.Mwinyi alitolea mfano wa tukio la wizi wa fedha lilitokea ZRB kupitia mfumo wa mtandao, ambalo hadi sasa halijaainishwa hatua zilizochukuliwa na kusema utamaduni huo umefanya vitendo kama hivyo kujirejea mara kwa mara.
Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande baada ya kusikiliza yaliyojiri na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi anakushirikisha jambo kupitia ushairi huu, karibu;

1:Zenj pesa nyingi sana, CAG akieleweka,
Wafujaji kuwabana, wale wanaeleweka,
Upotevu kutoona, ripoti mwaka kwa mwaka,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

2:Usimamizi mzuri, bajeti vema kushika,
Manunuzi bila shari, bei za kueleweka,
Muda mfupi subiri, hali itavyoboreka,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

3:Kweli wala hatanii, wezi bora kukumbuka,
Dumisha wenu utii, kwa vema kuwajibika,
Tusibaki hali hii, nchi iweze inuka,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

4:Isije kuonekana, yalopita yasikika,
Wizi na kuzungushana, kukome na kukatika,
Fedha tuweze kuona, mazuri yakitendeka,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

5:Msikiao sikia, haya yanaeleweka,
Rais keshawambia, vema yake kuyashika,
Mkizidi kurubia, wizi mtaaibika,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

6:Serikali yahitaji, fedha zinazotajika,
Bajeti kwake mtaji, miradi kukamilika,
Kukiwa na ufujaji, mwisho haiwezi fika,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

7:Kwa wakaguzi wa ndani, zidini kuwajibika,
Mfanye ndani kwa ndani, yale ya kushaurika,
Hasara mabilioni, ziweze sahaulika,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

8:Tena juzi kapandisha, mshahara kasikika,
Tena amenufaisha, wote kimeeleweka,
Hiyo hamasa yatosha, kwa wema kuwajibika,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

9:Ujenzi, Kilimo, afya, wamekwishawamulika,
Kidogo kama mwabofya, mjue tutawashika,
Wizi wote piga chafya, kwenu uweze toweka,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

10:Taasisi zote dola, ujumbe umewafika,
Wale hovyo wanakula, ni vema mkawashika,
Mahakama pia jela, zipo watawajibika,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

11:Dokta umesikika, wapenda kuwajibika,
Ufanyayo twayashika, kesho yasijetutoka,
Tuhakiki yafanyika, wizi uweze toweka,
Rais amepania, wizi wote kukomesha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, baada ya kukabidhiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar tarehe 27 Agosti 2022 na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news