Tuwe na chombo ambacho kinatuunganisha Serikali na wadau wa habari-Balile

NA MWANDISHI WETU

BAADA ya haki ya uhai, haki inayofuata ni haki ya kupata habari na suala la habari halihitaji mipaka ya nchi.
Hayo yamebainishwa Agosti 6, 2022 na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile wakati akizungumza katika Kipindi cha Mezani kinachorushwa na Kituo cha Redio cha EFM jijini Dar es Salaam.

Amesema, haki ya uhai haipo kwenye mikono ya mwanadamu yeyote lakini haki ya habari inapangwa na wanadamu namna ya kuitumia.

“Tunataka sheria hizi za habari zitupe mwongozo wa msingi. Baada ya haki ya uhahi, kinachofuata ni haki ya kupata habari,” amesema Balile wakati akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini.
Na kwamba, duniani kuna mifumo mitatu ya usimamizi wa vyombo vya habari, ambapo kila serikali huamua kuchagua mfumo mmoja kati ya hiyo.

“Kuna mfumo wa kwanza ni self regulation (kujitathmini), mfumo wa pili ni serikali ‘kushika’ vyombo vya habari kama ilivyo sasa na mfumo wa tatu ni co-regulation ambapo serikali na wadau wa habari wanakuwa na chombo ambacho kinawaunganisha.
“Sisi tunataka huu mfumo wa tatu ambao ndio tunaupigania, sio ule wa serikali kuwa mlalamikaji, msuluhishi na hakimu. Huu mfumo utazikwa kwa kuunda Baraza Huru la Vyombo vya Habari,” amesema Balile katika Kipindi cha Mezani kinachorushwa na Kituo cha Redio cha EFM, jijini Dar es Salaam.

Amesema, TEF kwa kushirikiana na wadau wa habari nchini, wanapendelea mfumo wa tatu ambao unatoa fursa kwa pande zote mbili (wadau na serikali) kuwa na sehemu ya kukutana pale kunapokuwa na malalamiko.
Akizungumzia ushirikishwaji wa wanahabari wenyewe kwenye mabadiliko hayo, Balile amesema wamekuwa na mikutano ya mara kwa mara na wanahabari katika kuwafafanulia vifungu hivyo.
Na kwamba, TEF imekuwa ikifanya mikutano na wahariri, waandishi pamoja na waandishi wa habari za mitandaoni (online media).

“Vikao hivi tumevifanya mara kwa mara na waandishi wanaelewa, na hatua iliyopo sasa ni kwenda kwenye mjadala ulioitishwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tarehe 11 – 12 Agosti mwaka huu kwa ajili ya kupitia vifungu vinavyolalamikiwa,”amesema Balile.

Post a Comment

0 Comments