Ujazi wa fedha nchini waendelea kuongezeka,MPC yaridhishwa na ukwasi wa kutosha katika mabenki

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (MPC) imeeleza kuwa, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi umeongezeka kwa kasi ya kuridhisha na kufikia wastani wa asilimia 9.9, sanjari na lengo la mwaka 2021/22.
Wakati huo huo, kamati hiyo imebainisha kuwa, ujazi wa fedha umeendelea kuongezeka sanjari na lengo la ukuaji kwa mwaka 2021/22, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera wezeshi ya fedha na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga baada ya kamati hiyo kufanya mkutano wake wa 221 tarehe 5 Agosti 2022 ili kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi kwa mwezi Mei na Juni 2022.

Prof.Luoga amefafanua kuwa, kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha, uliopelekea kuwepo ukwasi wa kutosha katika mabenki, na hivyo kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

Hata hivyo, amesema kuwa kamati imeendelea kufuatilia kwa karibu ongezeko la mfumuko wa bei kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, hali ambayo inaweza kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi nchini

“Pia utekelezaji wa sera ya bajeti kwa mwaka 2021/22 ulikuwa wa kuridhisha, huku viwango vya ukusanyaji wa mapato vikiendelea kuongezeka.

“Sekta ya nje imeendelea kukabiliwa na changamoto za ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia, na athari za Benki Kuu katika nchi mbalimbali duniani kuanza utekelezaji wa sera ya fedha yenye kupunguza ukwasi ili kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei,”amefafanua Prof.Luoga.

Fedha za kigeni

Hata hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubakia katika viwango vya kuridhisha, kutosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi 4.6 mwezi Juni 2022. Mwenendo huu umeendelea kuchangia utulivu wa thamani ya shilingi nchini.

“Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania na dunia, Kamati ya Sera ya Fedha, imeridhia Benki Kuu ya Tanzania kupunguza kasi ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi katika nusu ya pili ya mwaka 2022, ili kukabiliana na athari za ongezeko la mfumuko wa bei, bila kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi.

“Aidha, kamati imesisitiza umuhimu wa Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, ili kuendelea kudumisha utulivu wa thamani ya shilingi na kulinda uchumi dhidi ya athari za kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia,”amefafanua Prof.Luoga.

Uchumi

Kamati imebainisha kuwa, uchumi wa dunia umeendelea kukabiliwa na athari za vita nchini Ukraine, kuibuka upya kwa maambukizi ya UVIKO-19 nchini China, ongezeko la mfumuko wa bei, pamoja na mazingira magumu ya kifedha katika soko la dunia.

Prof.Luoga amebainisha kuwa, athari hizi zimeendelea kudumaza kasi ya kuimarika kwa uchumi wa dunia na hivyo kupelekea Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kushusha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2022 na 2023, ikilinganishwa na makadirio ya awali.

Pia mwenendo wa hali ya uchumi katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022, umebakia sambamba na makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2022 wa asilimia 4.7 na asilimia 5.4 kwa Tanzania Bara na Zanzibar, mtawalia.

"Mfumuko wa bei uliongezeka kufikia asilimia 4.0 na asilimia 4.4 mwezi Mei na Juni 2022, mtawalia, kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa kutoka nje ya nchi, japo umebaki ndani ya lengo la asilimia 3-5 kwa Tanzania Bara na asilimia 5 kwa Zanzibar.

"Aidha, kasi kubwa ya kuendelea kuongezeka kwa bei za chakula, nishati na mbolea katika soko la dunia, zinaashiria uwezekano wa ongezeko la mfumuko wa bei nchini kwa siku za usoni,"amefafanua Prof.Luoga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news