WAFUNGWA BADO NI WATU:Malezi mema yadumu, jela kuwe na nidhamu

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

AGOSTI 29, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amemuagiza Kamishna Jenerali mpya wa Jeshi la Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka kuhakikisha haki za wafungwa zinalindwa magerezani ikiwemo malazi na chakula.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Mzee Ramadhani Nyamka kuwa Mkuu wa Jeshi hilo katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 29 Agosti, 2022.
 
Pia Mheshimiwa Rais Samia amewataka majaji aliowaapisha katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, wafungwa bado ni watu, hivyo jela kuwe na nidhamu.

Maono hayo yanaenda sambamba na majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ambalo ni kuwapokea na kuwahifadhi gerezani watu wote wanaopelekwa gerezani kwa mujibu wa sheria za nchi na kuendesha programu mbalimbali zenye kulenga kuwarekebisha wafungwa waliohukumiwa ili hatimaye watoke gerezani wakiwa raia wema.

Katika kutekeleza majukumu hayo Jeshi la Magereza linawajibika kufuata na kuheshimu sheria zote za nchi pamoja na sheria mbalimbali za kimataifa zinazohusu haki za binadamu, jifunze jambo kupitia shairi hapa chini;

1:Wafungwa ni wanadamu, haki zao ni muhimu,
Huko pokea salamu, msidharau heshimu,
Zali hufika kwa zamu, wanakumbwa wanadamu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

2:Ameshatuma salamu, Rais wa kwetu humu,
Wale tumewahukumu, wakafanye kazi ngumu,
Haki zao tuheshimu, wanabaki binadamu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

3:Jeshi Magereza dumu, kutengeneza nidhamu,
Wafungwa wenye wazimu, na makosa kuyazumu,
Iwaingie fahamu, waishi kibinadamu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

4:Weledi siwe adimu, kuwatunza wanadamu,
Malezi mema yadumu, jela kuwe na nidhamu,
Wafungwa wakihitimu, wawe bora binadamu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

5:Vile wale wanadamu, nguo nzuri wana hamu,
Hata kuona filamu, jioni wakijihimu,
Chakula kile kitamu, hewa safi siyo sumu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

6:Jela kukaa kugumu, hilo bora tufahamu,
Kutenda mema muhimu, kukwepa hizi hukumu,
Uraiani udumu, raia mjenga timu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

7:Rais yuko timamu, kwa haki za binadamu,
Afanya zamu kwa zamu, kufanya yanayodumu,
Wito alotoa humu, Ilani ya SiSieMu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

8:Kuna Ibara muhimu, Ilani ya SiSieMu,
Kwamba haki ni muhimu, kwao wote wanadamu,
Rais Samia dumu, kuhakiki twaheshimu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

9:Kwenda jela siwe hamu, kufungwa siyo kutamu,
Makosa jinai sumu, hukumu zisije dumu,
Tubakie huru humu, huku tukijiheshimu,
Japo wanaadhibiwa, wafungwa bado ni watu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news