Waziri Bashungwa:Serikali, taasisi za kidini tutazidi kushirikiana kuibua fursa kwa vijana, wananchi

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini kuweka mazingira rafiki na bora kwa ajili ya vijana na wananchi katika kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kuleta maendeleo endelevu katika Taifa.
Ameyasema hayo leo Agosti 7, 2022 wakati wa akifunga Kongamano la Tano la Taifa la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania (VIWAWA) lililofanyika mkoani Tabora na kuwakutanisha vijana wapatao 2,535 kutoka mikoa ya Tanzania na nchi za nje kwa lengo kukutana kujifunza na kuimarisha ushirikia wa vijana.

Bashungwa, amesema Serikali inatambua changamoto wanazokumbana nazo vijana katika juhudi za kutafuta maisha bora ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, nyenzo za kilimo, masoko ya bidhaa, mikopo kwa ajili ya shughuli za biashara, nafasi za uongozi katika jamii na ushirikishwaji katika vyombo vya maamuzi.
Amesema, Serikali kwa kutambua umuhimu wa vijana, inaendelea kutengeneza fursa nyingi ikiwa ni utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ambapo katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2021, jumla ya shilingi bilioni 53 zilikopeshwa kwa vikundi 7,993 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha, Bashungwa ameeleza Mpango Kabambe wa Kushirikisha Vijana katika Kilimo Biashara ambapo Serikali imejipanga kutekeleza, uanzishwaji wa maeneo maalumu kwa ajili ya vijana waliopo katika kilimo biashara, uanishaji wa maeneo yatakayoboreshwa na miundombinu (block farms), mafunzo kwa vitendo, kuanzishwa kwa mifuko wa vijana, vile vile zaidi ya hekta 77,000 za ardhi ya umwagiliaji zitatengwa kwa ajili ya vijana kupitia skimu.
Pia, Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa bima za afya na huduma za vijana mbapo mwaka 1996 ilianzisha utaratibu wa malipo kabla ya kuugua, katika sekta rasmi na isiyo rasmi,

Katika sekta isiyo rasmi, Mfuko wa Afya ya Jamii ulilenga kuwafikia asilimia 80 ya wananchi, kwa kuanzisha mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), kwa Sheria ya mwaka 2001.

Wakati huo huo,Waziri Bashungwa amefafanua kuihusu ushirikishaji wa vijana kwenye maamuzi na uongozi katika nafasi ambapo Serikali imekuwa ikiruhusu kwa mujibu wa katiba, kila raia aliyefikisha umri wa miaka 18 kushiriki katika kupiga au kupigiwa kura kadiri ya utaratibu uliowekwa katika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwateuwa vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Taasisi,” amesema Bashungwa.

Vile vile, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutoa mikopo kwa vijana wote wenye sifa za kupata mikopo kwa elimu ya juu, kulingana na bajeti inavyoruhusu na itaendelea kuongeza juhudi na mfumo wa upatikanaji wa mikopo, pamoja na elimu bora kwa wote.

Amepongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kwa kuendelea kuhimiza maadili, malezi, uzalendo, uwajibikaji na kulinda utu kwa vijana na Taifa na akahimiza uchangiaji wa ujenzi wa kituo cha malezi ya vijana ambapo amehaidi kuchangia shilingi milioni tano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news