Waziri Nape, Balile: Tunakwenda hatua ya pili,wadau wa habari tunafarijika

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeonesha utofauti wa kipekee katika kuyafanyia kazi mahitaji ya wadau wa habari nchini.

Miongoni mwa mahitaji yao ni pamoja na utayari wa kukubali kuyapokea mapendekezo ya maeneo ambayo yanaonekana kuwa kikwazo kwa tasnia hiyo kupitia Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ili yaweze kufanyiwa maboresho, baada ya pande mbili kwa maana ya Serikali na wadau kukubaliana kwa pamoja.

"Mapendekezo ni mengi, lakini zamu hii iko tofauti kidogo na zamu zilizopita nasema hivyo kwa sababu mwaka 2014, 2015 na 2016 sisi tulikuwa tukipeleka mapendekezo tunayaona yakishafika bungeni. Lakini zamu hii Serikali imekuwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo imeamua kutushirikisha wadau kabla ya kwenda bungeni.

"Ikasema kwamba, kuna vifungu hivi, sisi tuna mawazo haya, kwa mfano kuanzia kifungu cha 38 tulikuwa na mapendekezo 20, lakini ukianzia kifungu cha 38 mpaka 67 kwa kweli tuwe watu wa shukrani.

Serikali imekubali

"Kwamba, Serikali yaliyo mengi imeyakubali na imezungumza kwamba haya mambo yana logic, lakini tumebaki na vifungu vichache sana ambavyo tunajaribu kuzungumza bado kwamba tunadhani kama tumerekebisha kuanzia 38 kwenda 67 basi ni vema tupitie tena kuanzia kifungu cha 1 hadi 37.

"Yale yanayoonekana kikwazo basi tuyarekebishe, lakini pia katika majadiliano kuna 'given take', kwa mfano sisi tulikuwa na hoja kwamba hivi vyombo vinne vibaki viwili. Idara ya Habari Maelezo, Baraza Huru la Vyombo vya Habari, Mfuko wa Mafunzo na Baraza la Ithibati, hivi vitatu vingeungana kiwe kimoja.

"Lakini katika mjadala ikaonekana kwamba ni vyema tukaondoa na sisi kama Serikali yenyewe imekubali kuanzia 38 imerekebisha mambo kadhaa kwa mfano zile minimum sentence, kashfa, sasa sisi tukiendelea kushikilia fungu lile lile tutaonekana kama hatukuingia kwenye mjadala.

Changamoto

"Ndio maana tukasema tunaendelea kuzungumza, tunaendelea kuomba na tukamwambia Mheshimiwa Waziri, akasema bado tunaendelea kuzungumza hatujafika mwisho. Kwa mfano kifungu cha 9 ni kati ya vifungu ambavyo vinatupa shida kwamba, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ana mamlaka ya kutoa leseni, kusitisha leseni, kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na kusimamia utekelezaji wa hukumu.

"Tunadhani katika mimbari au misingi ya utawala bora hili linahitaji nalo kurekebishwa, lakini zamu hii hatushikani mieleka tunakwenda kuzungumza hoja kwa hoja. Na linaloeleweka linarekebishika na hata tusipokubalina tunakuwa tunajua kwamba, kwa kweli kuna sababu ya msingi iliyofanya tusikubaliane,"amefafanua Bw.Balile.

Utofauti

"Serikali ya Awamu ya Sita ina utofauti kidogo na iliyopita...simu yako ilikuwa ukipigiwa unaweka VPN kwanza unapiga kwa WhatsApp, lakini kwa sasa hivi hata tunavyojadiliana hivi hii fursa haikuwepo kipindi kilichopita, lakini kwa sasa mnakaa mnazungumza mnakubaliana...mwelekeo huu wa kuendelea kuzungumza unatufanya tuone mwelekeo mzuri.

"Kwa mfano tumezungumzia kifungu cha 38, ilikuwa mwandishi sheria inasema atafungwa si chini ya miaka mitatu maana yake ni kwamba Hakimu anaweza kuamka asubuhi amepiga mtindi akamfunga 200. Lakini hilo Serikali imeliona imeliondoa kwa hiyo tunazungumza kwa mfano tumekwenda mambo kama universal peer mechanism
tukakubaliana kama nchi turekebishe hapa sheria hii ilete manufaa kwa taifa.

Si upendeleo

"Kwa hiyo hata sisi tunapozungumza hatuzungumzi kwa ajili ya kutaka kupendelewa kama vyombo vya habari tunataka haki na wajibu kwa sababu hata sisi tusipowajibika tunaweza kujikuta tunakwenda sehemu ambayo haikutarajiwa kama nchi.

"Mwanzo kasi ilikuwa nzuri sana, katikati ikalegea kidogo, lakini huu mwezi tuliopo kasi imeongezeka na tunadhani kwamba Mheshimiwa Waziri amekuwa akisema mara kadhaa kwamba anahakikisha mwaka huu kuna kitu kitatokea.

"Yapo mambo mengi ya msingi ya kuyafanyia kazi na tunasema unapodai haki lazima uwe na wajibu, kwa mfano kuna eneo moja huu msimamo wa Jukwaa la Wahariri ni tofauti na baadhi ya taasisi zingine.

Kiwango cha elimu

"Tunasema kwamba kiwango cha elimu sisi tunaamini kwamba angalau mtu awe na degree ya kwanza kufanya kazi ya uandishi wa habari.

"Wapo wenzetu wanasema, kila anayejua kusoma na kuandika anaweza kufanya kazi ya uandishi wa habari sisi tunasema tunakaa news room (vyumba vya habari). Tunasimamia vyombo vya habari tunaona madhara ya watu kuja bila elimu,makosa yanayofanyika kwenye mikono bila watu kuwa na kiwango stahiki cha elimu.

"Kwa hiyo sisi hapa tunasema kwamba kuongeza kiwango cha elimu ni haki kabisa tunapenda, tunatarajia hata hivyo wale wanaojiita Social Media ambao wanasababisha kelele nyingi mpaka kimataifa na wenyewe basi tuwe na miongozo sio mtu akiamka asubuhi sababu anajua kusoma na kuandika anafanya kazi hiyo.

Socia Media

"Kipindi cha nyuma tulishuhudia ikitokea ajali watu wanapiga picha, utumbo umemwagika barabarani ana-publish kwenye Social Media. Kama na wao hawatakuwa na hiyo Diploma (Stashahada) au degree (Shahada) wawekewe kiwango fulani walau cha maadili ambayo akiyakiuka awe na wajibu wa kuwajibika.

"Nia ya vyombo vya habari ni kutumikia wananchi, na nchi yetu. Tanzania ndio nyumbani kwetu hapa. Hakuna atakayesoma gazeti ukianzisha vita wakati anakimbia na mzigo kichwani, wala kusikiliza redio wala TV kwa hiyo sisi tunajenga nchi yetu tunashirikiana na Serikali na wananchi kujenga nchi yetu. Serikali ikifanya jambo jema tuishukuru ikifanya lisilo jema tuikosoe kitaaluma ni vyema,"amesema Balile.

Waziri Nape

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye amesema kuwa, "Kwanza niseme kwamba kinachofanyika sio kutunga sheria, kinachofanyika ni kurekebisha sheria na marekebisho ya sheria yameanza baada ya malalamiko kwa maana ya wadau watekelezaji wa sheria kusema hii sheria inatusumbua wengine wakaenda mahakamani, tukawaambia leteni mapendekezo mnayodhani tufanyie mabadiliko kama Serikali.

"Wakaleta jedwali kubwa sana, Jukwaa la Wahariri, wanasheria ilikuwa ni mchanganyiko wa mawazo ya wadau wengi wakaleta, Serikalini tukayachambua yale mapendekezo waliyoleta. Tuliyoyachambua tuliyoyachambua tukatengeneza na sisi jedwali lililoonesha mtazamo wa Serikali na nini tunadhani ndicho kiwe baada ya kufanya huu uchambuzi.

"Wakaenda kukaa kikao cha kwanza, kikao kile wakajadiliana sasa mawazo yao ni haya, mawazo ya serikali ni haya wakajadiliana mpaka wakafikia walipofikia.

Hatua ya pili

"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Dhamira ya sheria

Amefafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.

"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana.

"Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona, kwa hiyo Serikali ipo tayari, kikao cha kwanza kimeenda vizuri na nimeridhika,sasa tutakwenda kikao cha pili ambacho nitalazimika kwenda mwenyewe tukae pamoja tuzungumze tujenge hoja, wanawaza nini, tunawaza nini mwishowe tutakubaliana, nchi ni yetu wote,"amesema Mheshimiwa Nape.

Wadau

Kwa nyakati tofauti wadau wa habari wakiwemo wananchi wameieleza DIRAMAKINI kuwa, kauli ya Mheshimiwa Waziri Nape kwamba hawataenda bungeni hadi wakae pamoja wakubaliane na pande zote kwa maana ya Serikali na wadau wa habari inadhirisha ni kwa namna gani Serikali ya Awamu ya Sita inavyothamini na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania.

"Mheshimiwa Waziri Nape ametoa maneno ya faraja sana, yanatupa nguvu, si sisi wananchi tu, bali kwa taasisi za habari ambazo kwa namna moja au nyingine tunaamini itajenga na kuimarisha umoja ambao utawezesha sisi wananchi kupata taarifa nzuri na za kichunguzi ambazo zitaleta majawabu ya changamoto zinazotukabili,"amesema Herman Julius mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam.

Rais Samia

Mei 2,202 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari nchini zirekebishwe.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.

Rais Samia pia alishauri waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa kuandika mambo mazuri ya kutetea Bara la Afrika huku akiwataka waandishi wa habari kuzitangaza mila na desturi nzuri za Tanzania.

“Tunazo mila na desturi tunapaswa kuzilinda, na nyinyi waandishi wa habari mnatakiwa kuzilinda ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Baadhi ya watu wanaposti picha chafu mtandaoni, wanajianika mtandaoni, wengine wanafanya hivyo kwa kutojua madhara ya kufanya hivyo,"alisema Rais Samia.

Waziri Nape tena

"Wajibu wetu wa kwanza ni kusimamia utungaji huu wa sheria ufanyike vizuri na hapa tutakuwa tunajua kwamba marekebisho ya sheria hayafanywi na Serikali. Yanafanywa na Bunge kazi ya Serikali ni kupeleka mapendekezo bungeni halafu yakipitishwa tunatunga sheria.

"Kazi itakayofuata ni kutengeneza kanuni ambazo zitaendena na sheria ambayo imetungwa na mle ndani kuna mambo mengi ya kufanya na mle ndani kuna mchakato ambao hatuusemi sana, mchakato wa kupitia Sera ya Habari.

"Katika nchi yetu ambayo ni msingi mzuri wa kuwa na sheria nzuri kwa hiyo tukaona yote kwa pamoja yaende pamoja, sera inachakatwa na sheria inachakatwa hili la kwanza. La pili hili ni kubwa sana, katika kila utawala uongozi lazima pawepo na political will (utashi wa kisiasa), huo utashi wa kisiasa ndio unaoleta amani na utulivu.

Tii sheria

"Nimewahi kusema haijalishi sheria hizi zinazopigiwa kelele...bado zipo hazijafutwa zinaweza kutumika na zikitumika hakuna mtu atahoji sababu zipo na zimetungwa. Actually kutozitumia inaweza kusababisha kuhojiwa, lakini nikawaambia kwa sababu ya nia njema ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya uumini wa dhati wa uhuru na wajibu wa wanahabari.

"Baadhi ya mambo amesema mnaweza mkanyamaza nayo mfano yako magazeti yanaendelea kuchapa hayana leseni leo tunavyoongea kwa nini, kwa sababu hawafikii vigezo vinavyotakiwa na sheria, lakini tukasema sheria yenyewe ambayo ingewapasa wafungiwe inalalamikiwa hebu waacheni waendelee.

Dhamira ya Serikali

"Nia ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri watu watimize wajibu wao, kwa hiyo ikitokea tatizo tunakutana tunakaa mezani hili jambo tunadhani haliko sawa.

"Tunadhani approach hii imesaidia kuwarekebisha wengi, mimi ni muumini wa Baraza Huru la Habari sio tu muumini kwenye hii sheria, mimi ni mwasisi kwa sababu tulipokuwa tunatunga hii sheria ya mwaka 2016 msingi wake ilikuwa kuangalia taaluma nyingine zinajisimamiaje.

"Na hapa lengo letu lilikuwa kupunguza mikono ya Serikali kwenye kusimamia habari, badala yake tuwaachie wanahabari wajisimamie wenyewe yabaki yale mambo ya msingi ya wajibu wa Serikali kulinda usalama wao, watu wake yale ya msingi yatabaki. Lakini haya ya kitaaluma hatuna sababu ya kuyaingilia ya kitaaluma yashughulikiwe na wanahabari wenyewe kwa sababu ndio wenye taaluma yao,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

"Wanawajibu wa kulinda taakuma yaonkama vile wanasheria, madaktari wanalinda heshima ya taaluma yao, wanahabari wanawajibu pia wa kulinda heshima ya taaluma yao.

Uwekezaji

"Wamiliki waangalie namna ya kuwekeza zaidi kwa mfano Tanzania ni kati ya moja ya nchi ambazo habari za kiuchunguzi zimeporomoka sana. Na habari za kiuchunguzi ni fedha wawezeshe watu waende wakachunguze hili ni la kwanza, pia kuangalia maslahi ya wanahabari, wanahabari wetu moja ya tatizo kubwa ni lililopo ni kwamba wanakuja kwenye habari kama chanzo cha kupata fedha (posho), lakini anayelipa ndio mpiga zumari ndiye anayeamua mziki uendeje.

"Lakini la tatu kupitia vyombo mbalimbali vitakavyoundwa pengine ni muhimu sana tukaendelea kujengeana uzalendo kwa sababu mara nyingi mtu anaweza akaandika amfurahishe msomaji, lakini bila kujali madhara yake yatakuwaje...kwa mfano mtu anapiga picha ya mtoto amepata ajali amefariki, hebu fikiria wewe ungekuwa mzazi wa yule mtoto picha yake inasambaa barabarani hili ni jambo la watu wakiambiana tukaondoka huko.

"Na hapa ndipo kuna hoja ya kuchora mstari kati ya wanataaluma na Citizen Journalist tuchore mstari fulani.

Uhusiano

"Kuhusu uhusiano wa vyombo vya habari binafsi na Serikali, Waziri Nape amesema uhusiano ni mzuri sana huku akitolea ushiriki wa vyombo vya habari vilivyohuska kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kujitokeza kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi nchini.

"Mimi Waziri mwenye dhamana ya habari nimefurahishwa na mahusiano yaliyopo, tumefanya kazi nyingi juzi tumeanza Sensa kama kuna sekta imefanya vizuri sana ni wanahabari wameshiriki kwa nguvu wako mbele wengine wameenda mbali zaidi kwa kufanya matamasha.

Kuhusu kasi ya maudhui yanayokwenda nje na utamaduni wa Mtanzania, Waziri Nape amesema kasi ya ukuaji wa Sayansi na Teknolojia ni hatari isipodhibitiwa, lakini Serikali akasema iko makini kuhakikisha inadhibiti hilo.

"Kasi ya maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ni kubwa sana kuna baadhi ya maudhui hata katika vyombo vyetu vya habari mfano leo nilikuwa nasoma kuna baadhi ya katuni zinahamasisha ushoga kama Serikali tuna wajibu wa kudhibiti cyber space ya Tanzania tuna mamlaka hiyo, utaona kwenye baadhi ya Social Media account zimefungwa sababu mtu ameonywa, lakini hataki juzi juzi tu kuna mtu ameandika Mwakyembe anaumwa, Mwakyembe amekufa, Mwakyembe amezikwa na amepublish Tv online na amesajiliwa kakutwa Morogoro...

Aidha, Waziri Nape amesema dhamira yake ni kuona tasnia ya habari inafanya vyema katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuhamasisha maendeleo, kujenga nchi uwajibikaji na Tanzania inakuwa kielelezo bora katika uhuru wa habari Kimataifa ili Dunia ijifunze kutoka Tanzania.

Amesema, tasnia ya habari iko salama nchini Tanzania kwani Mheshimiwa Rais Samia Hassan ni muumini mzuri wa haki na uhuru wa habari, hivyo wanahabari nchini na wadau wa habari waondoe shaka na yeye kama Waziri jukumu hilo amekabidhiwa atalifanya kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news