Wizara kuanzisha Tanzania Madini Marathon 2023

NA STEVEN NYAMITI

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini inatarajia kuanzisha mashindano ya mchezo wa mbio utakaojulikana kama ‘Tanzania Madini Marathon’ ifikapo Mwaka 2023 ili kuhamasisha watanzania kushiriki katika michezo maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 14, 2022 na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko baada ya kushiriki Shinyanga Madini Marathon iliyofanyika mkoani Shinyanga.

Aidha, Dkt. Biteko amesema mwaka 2023, Serikali itaifanya Tanzania Madini Marathon kuwa ya kitaifa kwa kuwakutanisha wadau wa Sekta ya Madini na Sekta nyingine ili kushiriki kwa pamoja.

Vile vile, ametumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema kwa kuandaa vizuri Shinyanga Madini Marathon ambayo imekuwa ya kwanza hapa nchini kuanzishwa.
Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko ametoa tuzo, medali na zawadi kwa washindi mbalimbali wa mbio fupi na ndefu, mbio za kukimbia na beisikeli pamoja na mashindano mengine ambao wamefanya vizuri na kumaliza mashindano.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mjema ameipongeza Wizara ya Madini kwa kushirikiana pamoja katika shughuli hiyo katika mkoa huo. Amesema kupitia marathon hiyo imeweza kuweka ukaribu wa Serikali na wananchi katika kufanya mazoezi ili kujenga mwili.
Shinyanga Madini Marathon 2022 imekuwa ya kwanza kuanzishwa hapa nchini katika Mkoa wa Shinyanga na kuwakutanisha wadau mbalimbali kushiriki katika michezo kuanzia mbio za km 21, km 10, km 5 na km 2.5, mbio za beisikeli na michezo mingine katika uwanja huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news