Wizara ya Afya yamfutia deni la Milioni 9/- mwanafunzi Lightness

NA CATHERINE SUNGURA-WAF

WIZARA ya Afya imemfutia deni la milioni 9 mwanafunzi Lightnes Shurima ambalo alikua akidaiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kutokana na matibabu ya Marehemu Baba yake aliyekua anatibiwa hospitalini hapo.
Aidha, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amemtaka mwanafunzi wa chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Hombolo Mkoani Dodoma Lightness Shirima kufika hospitali ya Taifa Mhumbili-Mloganzila na kuonana na Mkurugenzi wa hospitali hiyo kesho tarehe 9 Agosti, 2022 kuchukua kitambulisho chake.

Waziri Ummy ameandika hayo kwenye mtandao wake wa kijamii na kueleza kwamba Serikali ya Rais Samia inatambua kuwa wananchi wengi ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu hususan katika kipindi ambacho matibabu yana gharama kubwa.

"Ili kutatua changamoto hii Serikali inakuja na Sheria ya Bima ya Afya kwa kila mtu (UHC) ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila ya kikwazo cha fedha".

"Ni matumaini yetu kuwa tukiwa na utaratibu huu wa Bima ya Afya kwa kila mtu (wananchi wengi wazima watachangiana kidogo kulipia wananchi wachache watakaokuwa wagonjwa tofauti na sasa ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wanaojiunga na Bima kwa hiari ni wagonjwa) masuala haya tutayapunguza kama siyo kuyamaliza kabisa".

Pia Waziri Ummy amerudia kuzitaka hospitali zote za Serikali nchini kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya kuwa kila baada ya siku chache kuprint bill ya mgonjwa(mteja) ili ndugu waweze kulipia na hiyo itasaidia kuwapunguzia mzigo wa kulipa bill kubwa za matibabu kwa mgonjwa wao.

Lightness Shirima hivi karibuni iliripotiwa na chombo kimoja cha habari kuwa anadaiwa milioni 9 deni ambalo aliliacha baba yake aliyefariki dunia katika hospitali hiyo na yeye kuacha kitambulisho cha NIDA kama dhamana.

Post a Comment

0 Comments