Afande Sele awaponza ZamaMpya TV,TCRA yawatoza faini milioni 2/-

NA DIRAMAKINI

KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeitoza faini ya shilingi milioni mbili runinga ya mtandaoni ya ZamaMpya kwa kosa la kuchapisha habari kuhusu tozo za Serikali bila kuzingatia maadili, hivyo kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Habbi Gunze akiwakabidhi hati ya hukumu wawakilishi wa Kituo cha runinga mtandaoni cha ZamaMpya baada ya kudaiwa kukiuka kanuni za maudhui ya utangazaji jijini Dar es Salaam.

Faini hiyo inatokana na kituo hicho kufanya mahojiano na msanii Seleman Msingi (Afande Sele) ambaye alikuwa akizungumzia masuala ya tozo bila kituo hicho kuzingatia maudhui ya utangazaji na maadili ya uandishi wa habari ya kuweka mizania ya habari.

Aidha, kituo hicho kimepewa onyo na kuwekwa chini ya uangalizi wa TCRA kwa miezi mitatu ili kuboresha utendaji kazi wao wa maudhui ya utangazaji

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Habi Gunze alisema Agosti 12, mwaka huu TCRA ilitoa leseni kwa ZamaMpya Tv na Agosti 28, mwaka huu walichapisha taarifa za uchochezi kuhusu tozo za serikali kwenye ukurasa wa Twitter kinyume na kanuni ya 9 (a), 12 (a) (I) na 16 (1) aya 3 (a), (d), (g), (h) na (k) ya kanuni za kielektroniki na Posta ya mwaka 2020.

Alisema, katika utetezi wa kituo hicho walikiri kuchapisha habari hiyo huku wakieleza kuwa walitafuta na kuchapisha habari hizo kulingana na katiba na kwamba hawajui kilichochochewa na madhara yaliyopatikana.

"Kituo hiki kimetenda kosa la uchochezi kwa kuchapisha maudhui basi yanayohusu tozo za serikali kwa kutuhumu viongozi bila kutoa nafasi ya kujibu, hivyo walikosa mizania. Pia taarifa yao haikuzingatia maadili na kanuni, kwani imesababisha kuhatarisha amani, umoja na usalama wa nchi," alisema Gunze.

Aliongeza kuwa TCRA ina mamlaka ya kulinda maslahi ya serikali na watumiaji wa mitandao hivyo, wana mamlaka ya kufuatilia kila taarifa inayochapishwa.

Alisema kituo hicho kimekosa umakini katika usimamizi wa maudhui kwa sababu taarifa kutoka kwa mtu mmoja yenye kuilenga serikali haipaswi kuchapishwa bila kufuatilia na upande wa serikali.

"Kwa kuzingatia Kanuni ya 21 (3) kamati inatoa adhabu ya faini ya shilingi milioni mbili ambazo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku 21 baada ya kusomwa hukumu hii, tunatoa onyo kali na tutaweka chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi mitatu ili kuhakikisha mnaboresha utendaji kazi wenu na haki ya kukata rufaa ipo wazi,"alisisitiza Gunze.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news