Afrika yaketishwa Tanzania kuangazia fursa za uwekezaji

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango,Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amefungua Kongamano la Uwekezaji barani Afrika linalofanyika jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo la siku mbili ambalo limeandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wakala wa Dhamana ya Uwekezaji wa Kimataifa (MIGA) ya Benki ya Dunia limefunguliwa leo Septemba 14, 2022 jijini Dar es Salaam.

Hili ni kongamano la kwanza kufanyika Tanzania na la pili barani Afrika katika muendelezo wa MIGA wa kuhamasisha na kuweka juhudi katika suala zima la kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara duniani.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba akizungumza katika kongamano hilo amewahakikishia washiriki wote kutoka ndani na nje ya Tanzania kuwa, Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji.
Pia amewashukuru MIGA kwa kuitisha kongamano hilo ambalo limewaleta pamoja viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Amesema,kongamano hilo ni jukwaa mahususi ambalo litawezesha kuibua mawazo mbalimbali na kushirikishana namna ambavyo sekta binafsi itashiriki vema katika kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Dkt.Nchemba amesema,kongamano hilo limekuja muda mwafaka ikizingatiwa Afrika inahitaji kuwa pamoja na kupiga hatua kimaendeleo ili kila nchi ifikie malengo yake kiuchumi.

Amesema,kutokana na changamoto mbalimbali za kidunia ikiwemo vita vya Ukraine na Urusi, majanga ya asili na UVIKO-19 uchumi wa Afrika umedhoofika, hivyo juhudi za pamoja kupitia biashara za kimataifa ni muhimu kwa ajili ya kukuza uchumi ikiwemo kutengeneza fursa za kimataifa, kukuza masoko, uzalishaji na kuzalisha ajira.

Waziri huyo amesema, kupitia biashara za kimataifa na mwingiliano una nafasi kubwa ya kuzidi kuimarisha uchumi wa mataifa, hivyo kuna haja kubwa ya kutengeneza mazingira ya kuwezesha uwekezaji na pia ameipongeza Benki ya Dunia kwa kuendelea kusaidia juhudi mbalimbali za kufanikisha mapambano ya umaskini na janga la UVIKO-19.

Pia amesema, rasilimali za asili zilizopo Tanzania ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi na kwamba serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha kila mmoja ambaye ana shauku ya kuwekeza Tanzania anapata huduma bora kwa wakati.

Naibu Katibu

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi.Amina Khamis Shaaban amewapongeza washiriki wa mkutano huo kutoka ndani na nje ya Tanzania huku akisema kuwa,hiyo ni heshima kubwa kwa Taifa.
Amesema,lengo muhimu la kongamano hilo ni kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji na wadau mbalimbali kwani wawekezaji watakutana na wawekezaji wakubwa kutoka makampuni makubwa barani Afrika na kutoka nchini mbalimbali duniani.

‘’Nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa kuonesha imani kubwa kwa Tanzania, wengi wenu hii ni mara ya kwanza kufika Tanzania, karibuni sana Tanzania, Taifa la amani.

"Ushiriki wenu katika mazungumzo haya utakuwa na tija kubwa sana na kuleta pamoja wawekazaji katika kuchochea ukuaji, ambapo mjadala utahusisha watu kutoka sekta mbalimbali binafsi na makampuni, na pia kutazama madhara ya janga la Corona ambapo Afrika iliathiriwa na janga hili pia,"amesema.
Pia amesema,kutokana na athari za janga la UVIKO-19 uchumi wa Afrika uliathirika kwa kiwango kikubwa ikiwemo kudhoofisha uzalishaji viwandani na miradi mbalimbali iliyokuwa ikitekelezwa.

TPSF

Raphael Maganga kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) amesema kuwa, kongamano hilo lina umuhimu mkubwa kwao, ikizingatia kuwa umoja huo unaunganisha wawekezaji mbalimbali hapa nchini.
Amesema, TPSF inaunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza miradi mbalimbali ili kustawisha uchumi.

"Dhamira yetu ni kuhakikisha tunashiriki kukuza uchumi wa Taifa ili uweze kuboresha maisha ya watanzania,MIGA imekuwa kichocheo kizuri katika ukuaji wa uchumi na chanzo cha kuibua fursa mbalimbali za uwekezaji ili kukuza uchumi na kuondoa umaskini duniani.
"Sekta binafsi Tanzania inafanya vyema katika kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika fursa mbalimbali, hata hapa kwenye kikao kuna wawakilishi wa makampuni mengi kutoka sekta binafsi,"amesema.

Kongamano hilo limeenda sambamba na Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika uliofanyika kuanzia Septemba 12 hadi 14, 2022 kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa wanawake na vijana katika biashara ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini Tanzania ambapo umewakutanisha viongozi mbalimbali kutoka barani Afrika wakiwemo wanawake na vijana.
Aidha, katika huu mkutano wa MIGA wa Afrika ni mahsusi katika kujadili namna bora ya kuhakikisha nchi za Afrika zinapata uwekezaji mkubwa na endelevu na kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa bora ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuja barani Afrika kuwekeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news