Azam sukari kuingia sokoni kesho

NA GODFREY NNKO

IKIWA imepita zaidi ya miaka sita baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kumpatia hekari 10,000 za ardhi bure mfanyabiashara,Said Salim Awadh Bakhresa ili kulima miwa na kuzalisha sukari, hatimaye matunda ya kiwanda hicho yameonekana.

“Nitakupa hekari 10,000 za ardhi kwa ajili ya kulima miwa na kuanzisha kiwanda cha sukari, tena kitakuwa karibu na Dar es Salaam;

Hayati Dkt.Magufuli aliyabainisha hayo mwishoni mwa mwaka 2016 wakati akizindua kiwanda cha Bakhresa Products Limited kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema, ametoa ardhi hiyo ili Bakhresa alime miwa na kuzalisha sukari badala ya kuagiza nje, hatua ambayo itasaidia pia kukabili uhaba wa sukari nchini.

Siku hiyo hiyo, Rais Magufuli alimpongeza Bakhresa kwa kuwa mfano mzuri kwa wafanyabiashara wengine kwa sababu ametoa ajira kwa watu wengi na analipa kodi serikalini.

Kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa leo Septemba 4,2022 imeeleza kuwa,Azam Sukari kutoka kiwanda chake cha Bagamoyo Sugar Limited itaanza kuingia sokoni kesho Septemba 5, 2022.

"Habari njema! Azam Sukari kutoka Bagamoyo Sugar itaanza kupatikana madukani kuanzia siku ya Jumatatu, tarehe 05/09/202,"imeeleza taarifa hiyo fupi iliyotolewa na Bagamoyo Sugar Limited.

Kiwanda hicho ambacho kipo Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kinamilikiwa na mfanyabiashara Said Bakhresa ambapo utekelezaji wa mradi huo ulianza mara moja baada ya Hayari Dkt.Magufuli kumpatia eneo bure ili alitumie kujenga kiwanda cha kuzalisha sukari nchini na kuondoa utegemezi wa kuagiza sukari nje kila mwaka.
 
Hata hivyo, mafanikio haya ya kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari nchini ni matokeo ya utekelezaji wa sera na mikakati ambayo Serikali imeweka kuhakikisha wazalishaji wana mazingira mazuri ya kufanya upanuzi wa mashamba na wakulima kuongeza tija.

Ujio wa Bagamoyo Sugar Limited unaenda kuunganisha nguvu kwa viwanda vingine vya Kilombero  Sugar Company Ltd,Mtibwa Sugar Estate, Kagera Sugar Ltd, TPC Ltd na Manyara Sugar Ltd hivyo kuongeza uzalishaji ambao utalifanya Taifa kukabiliana na uhaba wa sukari kila mwaka.

Pia Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa wakulima wadogo ili viwanda viongeze uwezo wa kuchakata miwa inayozalishwa na kuongeza tija kwa uwepo wa mbegu bora na viuatilifu.

Post a Comment

0 Comments