Bima ya Afya kwa wote yaiva, Rais Samia asema mwezi huu kuna jambo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa, Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utapelekwa na kupitishwa bungeni mwezi huu, ikiwa Bunge litaanza vikao vyake Septemba 13, 2022 jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Maaskofu wa Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki wakati wa Jubilee ya miaka 50 ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) iliyofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Septemba, 2022.

“Nataka niwape habari njema kwamba Bunge litakalokaa mwezi huu wa tisa, linakwenda kupitisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa Watanzania wote.Niwaombe sana ndugu zangu, tutakapopitisha sheria hii, Watanzania twendeni tukajiunge na mifuko ya bima ya afya;

Amebainisha hayo leo Septemba 11, 2022 wakati wa hafla ya kilele cha kusherekea za Miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA).

Sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam huku akitoa wito kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya.

Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha mfuko utakaosimamia bima hiyo unafanya kazi kwa ufanisi na utasimamiwa na sheria na kanuni mpya.

“Nataka niwahakikishie, tunajua udhaifu wa mifuko yetu, tumechukua hatua tutakapoanza bima ya afya kwa wote mfuko utakaosimama kusimamia bima ya afya kwa wote utakuwa mfuko madhubuti wenye sheria na kanuni mpya ambazo zitafanya watu wote waweze kutibiwa katika viwango mbalimbali, mtu aweze kupata matibabu yote anayopaswa kupata,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Post a Comment

0 Comments