BODABODA MKOANI MARA: 'Sisi ndio wahanga, wanasiasa msituvuruge acheni Jeshi la Polisi lifanye kazi yake, tulichoka kuuawa, tulichoka kuibiwa bodaboda zetu'

NA DIRAMAKINI

WAENDESHA pikipiki maarufu bodaboda mkoani Mara wamefanya maandamano ya amani ya kulipongeza jeshi la Polisi mkoani humo kwa jitihada na jinsi linavyoendelea kukabiliana na vitendo vya kihalifu.
Maandamano hayo yamefanyika leo Septemba 28, 2022 kuanzia eneo la 'Musoma Bus' kwenda Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa zilizopo kata ya Mukendo Manispaa bya Musoma wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali za kutoa pongezi kwa IGP Camillus Wambura na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara namna ambavyo jeshi hilo limezidi kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.
Akisoma risala ya waendesha bodaboda hao Afisa Habari wa Bodaboda Mkoa wa Mara, Faustine Mbarouk amesema kuwa, jeshi hilo limeweza kuimarisha usalama kwa kiwango kikubwa mkoani Mara na hivyo kuwezesha kundi la waendesha boda boda kufanya kazi kwa amani tofauti na kipindi cha nyuma.
Faustine amesema kuwa, kwa kiwango kikubwa jeshi hilo limeweza kudhibiti vitendo vya wizi wa pikipiki na utekwaji wa waendesha piki piki na kuuawa ambapo vitendo hivyo kipindi cha nyuma vilishamiri, lakini kwa sasa waendesha bodaboda wanafanya kazi kwa amani na usalama kutokana na operesheni mbalimbali ambazo limeendelea kuzifanya ndani ya mkoa huo.
Ameliomba Jeshi la Polisi Mkoani Mara lisikatishwe tamaa na kauli za wanasiasa ambao wanaweza kutumia operesheni hizo kufanya upotoshaji kwa umma. Huku akisema kuwa waendesha bodaboda wataendelea kushirikiana na jeshi hilo kumaliza vitendo vya kihalifu kwa kutoa ushirikiano thabiti.

Ameongeza kuwa, jeshi hilo lisirudi nyuma kuwachukulia hatua wale wote wanaobainika kujihusisha na Vitendo vya kihalifu wakiwemo majambazi, vibaka kwani hatua hiyo itazidi kuwafanya wananchi waendelee na shughuli za uzalishaji mali kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waendesha Boda boda Wilaya ya Musoma Mjini Stephano Silas amewataka waendesha boda boda Wilayani humo kujisajili katika vituo halali vya kazi. Na kwamba, boda boda wote wafuate sheria na taratibu za nchi pia wasijihusishe na vitendo vya kihalifu ambavyo vitawafanya watiwe hatiani.

Amesema wanaokuja kufanya kazi ya boda boda Wilayani Musoma na Mkoani Mara kwa ujumala, wahakikishe wanafanya kazi hiyo kihalali, lakini wanaokuja na kuingia katika kazi hiyo wakiwa na agenda ya kufanya uhalifu amesema hawatafanikiwa kutokana na ushirikiano wao na Jeshi la Polisi.
Kwa Upande Wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Longinus Tibishubwamu akizungumza na Waendesha boda boda hao amewapongeza kwa uzalendo wao wa kutambua juhudi zinazofanywa na Jeshi hilo kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao.
Kamanda Tibishubwamu amesema, Jeshi hilo litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kusudi wafanye kazi saa 24. Huku akiwaahidi ushirikiano boda boda wote na wananchi wote mkoani Mara ili wafanye kazi za uzalishaji mali kwa amani na utulivu.

Post a Comment

0 Comments