Nkasi wajiweka tayari kwa ujenzi madarasa mapya ya Rais Samia

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Wilaya Nkasi mkoani Rukwa,Mheshimiwa Peter Lijualikali ameiagiza idara ya elimu na wahandisi wa wilaya kuanza kutengeneza gharama halisi za ujenzi kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa madarasa kama agizo la Serikali lililotolewa la ujenzi wa madarasa 8,000 nchi nzima.

Ni kupitia fedha zitakazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Ameyasema hayo leo Septemab 28,2022 kwenye kikao cha wadau wa elimu wakati akizindua miongozo ya elimu ngazi ya wilaya.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa, Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mheshimiwa Inocent Bashungwa imetangataza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 8,000 nchi nzima hivyo ni muhimu sasa kuendelea kufanya maandalizi ya ujenzi wa madarasa hayo.

Amesema kuwa, ni muhimu gharama za ujenzi zikajulikana mapema ili fedha zikitolewa kazi ianze mara moja na kukamilika kwa wakati kwa maana gharama halisi zitakua zinajulikana.

Wakati huo huo amewataka waalimu kusimamia vyema miongozo hiyo ya elimu kwani lengo lake ni kutaka kuleta mabadiliko katika sekta hiyo ya elimu na kubwa kusimamia maadili kama yanavyowaongoza ili kuweza kuyafikia malengo.

Awali Afisa Elimu Msingi, Augustine Bayo alisema kuwa miongozo hiyo ya elimu ipo ya aina tatu ambayo ni uteuzi wa viongozi wa elimu ngazi ya serikali za mitaa na mikoa,kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi na changamoto katika uboreshaji elimu ya msingi na sekondari.

Mwenyekiti wa Walimu Wakuu ngazi ya wilaya kupitia TAPSHA, Stivine Katiya kwa upande wake alimuhakikishia mkuu wa wilaya kuwa watakwenda kuisimamia miongozo yote ya elimu, lakini kubwa ni kutaka kuona ufanisi katika sekta hiyo ya elimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news