BoT:Tuna akiba ya fedha za kigeni ya kutosha kuagiza bidhaa, huduma nje ya nchi miezi 4.6

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imesema akiba ya fedha za kigeni nchini imeendelea kubakia katika viwango vya kutosha na kufikia dola za Marekani milioni 5,092 mwishoni mwa mwezi Agosti 2022, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takribani miezi 4.6.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florence Luoga ambapo amefafanua kuwa,Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imefanya kikao chake cha 222 Septemba 23, 2022.

Amesema, lengo la kikao hicho ni ili kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi kwa kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2022.

Pia amesema, kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha, uliotoa wigo wa kukuza shughuli za kiuchumi, licha ya kuwepo kwa changamoto zinazosababisha kupanda kwa mfumuko wa bei, kutokana na ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia.

"Kwa kuzingatia mazingira ya sasa na changamoto za kiuchumi duniani, Kamati ya Sera ya Fedha imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni ili kudumisha utulivu wa thamani ya shilingi na kukidhi mahitaji ya nchi.

"Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania na changamoto za kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani, pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa, Kamati ya Sera ya Fedha imeiridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kupunguza taratibu kasi ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi katika kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba 2022.

"Uamuzi huu unalenga kukabiliana na athari za kuendelea kuongezeka kwa mfumuko wa bei, sambamba na kulinda kasi ya ukuaji wa uchumi,"amefafanua Prof.Luoga.

Post a Comment

0 Comments