Bunda wafikiwa na mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia maeneo ya uvuvi

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara limezindua mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia maeneo ya uvuvi katika kata nne za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Mradi huo unatekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society ambapo kata za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda zinazonufaika na mradi huo ni pamoja na Kata ya Iramba, kasuguti, Chitengule na Nyamhiyolo.

Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba 27, 2022 makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yaliyopo Kata ya Kibara wilayani humo na kuhudhuriwa na viongozi wa halmashauri hiyo, Kamati za Usimamizi wa Mialo (BMU), viongozi wa dini pamoja na Maafisa Watendaji wa kata zinazonufaika na mradi huo.

Pia, Septemba 22, 2022 shirika hilo lilizundua mradi huo katika kata saba za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane katika Halmashauri zote mbili kuanzia Septemba 2022, hadi Aprili 2023 katika halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na utagharimu jumla ya shilingi milioni 37 kwa halmashauri zote.

Ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mradi huo utatekelezwa katika kata saba ikiwemo kata ya Bukima, Rusoli, Bukumi,Nyamrandirira, Bwasi, Msanja na Kiriba.
Meneja wa Shirika la VIFAFIO linalotekeleza mradi huo, Majura Maingu amesema, lengo la mradi huo katika halmashauri zote mbili ni kufikisha elimu ya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya mialo na visiwa ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kuilenga jamii ya wavuvi.

Amesema kuwa, mradi huo waliomba kwa mfadhili utekelezwe kwa miaka mitatu kwa thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 200 walizoomba lakini wamepewa shilingi milioni 37 watekeleze kwa kipindi cha miezi nane. Hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa maeneo husika ambayo mradi huo unatekelezwa ili uwe na tija kwa Jamii Kama.ivyokusudiwa.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Robinson Wangaso amesema kuwa, mradi huo utahusisha kutoa elimu kwa wavuvi maeneo ya mialo, kutumia michezo kutoa elimu, kufanya mikutano ya hadhara na wavuvi, kufanya majadiliano na wadau pamoja na kuunda klabu za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Amesema, mradi huo unatarajia kuleta matokeo ikiwemo kuwafanya wanawake na watoto wachukue hatua kwa kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kwa mamlaka za serikali na Jamii iwe na uwezo wa kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kuimarisha mfumo bora katika kamati za Vijiji na kata zinazohusika na kupinga vitendo hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Changwa Mkwazu akizungumza katika uzinduzi huo, amelishukuru Shirika la VIFAFIO kwa kutekeleza mradi huo katika Halmashauri ya Bunda kwani utaigusa Jamii na kuinufaisha wananchi.

Ameongeza kwa kusema kwamba, Serikali inatambua kwa dhati mchango wa maendeleo unaofanywa na mashirika yasiyo ya Kiserikali Katika kuwasaidia wananchi na hivyo kuunga mkono juhudi za serikali kwa vitendo Wilayani humo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mradi huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Charles Magafu amesema kuwa mradi huo umekuja muda muafaka kwani utasaidia kwa kiwango kikubwa kupambana na vitendo hivyo vya ukatili wa Kijinsia.

Amesema kwamba, maeneo ya mialo katika Halmashauri ya Wilaya hiyo yanakabiliwa na tatizo hilo la ukatili wa kijinsia ikiwemo kata yake anayotoka ya Iramba hivyo kupitia mradi huo utawezesha kuleta mabadiliko chanya kwa jamii ya wavuvi.

Aidha Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Fausta Parali amesema elimu ya kupinga ukatili wa Kijinsia itakayotolewa katika mialo wakati wa Mradi unatekelezwa iangazie elimu ya ulinzi, malezi na makuzi kwa watoto sambamba na kuhuisha na kutoa mafunzo kwa kamati za ulinzi na usalama wa Wanawake na watoto ili kudhibiti vitendo vya ukatili wa kimwili, kiuchumi, kisaikolojia na kiuchumi.
Padri Costantine Bigambo kutoka Parokia ya Kibara Jimbo la Bunda akizungumza wakati wa mjadala amesema Jamii iendelee kulinda haki za watoto, kuwathaminiwa, kuwapa elimu bora, matibabu, na haki zote zinazowahusu na kwamba, Wazazi na walezi wawape elimu ya ukatili wa kijinsia Watoto wao, na serikali iendelee kusimamia sheria na kanuni zinazowalinda kwa ufanisi.

Padri Costantine ameihimiza Jamii iendelee kuwa na mahusiano mazuri na Watoto, Jamii ijengewe uwezo kujua haki za watoto sambamba na kutumia sanaa, michezo maonesho maeneo ya mialo kutoa elimu ya ukatili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news