Bunge la Tanzania latangaza ratiba uchaguzi wabunge wa EAC

NA GODFREY NNKO

KATIBU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Nenelwa J. Mwihambi ambaye ni msimamizi wa Uchaguzi wa Wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki amesema kwamba, uchaguzi wa wajumbe tisa watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa mkutano wake wa Nane utakaoanza Septemba 13, 2022 jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 6, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge jijini Dodoma imeeleza kuwa, uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia kuwa,maisha ya Bunge la Afrika Mashariki lililoingia madarakani mwaka 2017 yatafikia ukomo wake Desemba 17, 2022.

"Msimamizi wa uchaguzi ametoa tangazo la uchaguzi huo katika Gazeti la Serikali la leo Septemba 6,200 kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni Septemba 20, 2022 saa 12 jioni.

"Na pia siku ya uchaguzi ambayo ni Septemba 22, 2022 saa tano kamili asubuhi, mara au mapema kabla ya muda wa maswali, wakati Bunge linaendelea na shughuli zake.

"Kwa taarifa hii, watu ambao wanazo sifa za kugombea na kuchaguliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki wanaweza kuanza mchakato wa kuteuliwa kuwa wagombea wa nagfasi hizo kupitia vyama vyao vya siasa,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, chama au mgombea aliyeshinda katika ngazi ya chama anapaswa kujaza fomu ya uteuzi inayotolewa na Bunge na kuiwasilisha kwa Katibu wa Bunge.

"Fomu hiyo imetangazwa katika gazeti la Serikali na inapatikana kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni www.bunge.go.tz,"imeongeza taarifa hiyo.

Post a Comment

0 Comments