Bweni la wavulana lateketea kwa moto Mara Secondary School

NA FRESHA KINASA

BWENI linalotumiwa na wanafunzi wavulana wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Mara iliyopo Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara limeteketea kwa moto wakati wanafunzi wakiwa darasani wakiendelea na masomo huku chanzo kikiwa bado hakijafahamika.
Viongozi wakielekea kukagua. (Picha na DIRAMAKINI).

Bweni hilo limeungua leo Septemba 9, 2022 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt.Halfani Haule amefika shuleni hapo akiwa na viongozi mbalimbali na kujionea hali hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Dkt.Haule amemuagiza Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere kufanya uchunguzi wa bweni hilo ili kujua chanzo chake.

Aidha, katika tukio hilo ambalo limeshuhudiwa na DIRAMAKINI, kikosi cha zima moto na uokoaji Mkoa wa Mara kilifika haraka na kuzima moto huo kabla ya kuteketeza mabweni mengine yaliyoko jirani na bweni hilo huku kukiwa hakuna mwanafunzi yeyote aliyepata madhara ya kuungua.
Viongozi wakikagua baadhi ya vifaa vya wanafunzi vilivyoteketea kwa moto. (Picha na DIRAMAKINI).

Katika tukio hilo, vifaa vya wanafunzi kama vile madaftari, vitabu, taulo za kiume, dawa za miswaki na magodoro yameteketea kwa moto huku thamani yake ikiwa bado haijafahamika.

"Mtapokea wageni wengi watakuja kuona athari za moto huu na kupata ufumbuzi niwape pole sana wanafunzi kwa tukio hili, lakini Serikali ipo pamoja nanyi.
"Tunaomba utulivu muda huu mchache tutaendesha zoezi la uchunguzi kujua nini kimesababisha ule moto kwenye lile bweni. Kama Kuna mtu unamfahamu amefanya hivyo toeni taarifa kwa Mwalimu. Jeshi la Zima Moto tunawapa mpaka kesho muwe mmeanza kufanya uchunguzi, pili tutafanya tathimini kujua vitu vilivyoungua kwa ujula gharama yake na tatu ni mpango wa dharura kujua wanafunzi mnasoma vipi, tumeona mna kompyuta room mtahamia mle ili kusudi kupisha ukarabati wa lile bweni,"amesema Dkt.Haule.

Wakati huo huo, Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Marwa Mathew akizungumza na wanafunzi hao ameahidi kutoa magodoro yote yaliyoungua kwa moto kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo ili kuwanusuru wanafunzi hao.
Amewataka kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa jambo hilo na kuwahimiza kusoma kwa bidii kuondoa shaka kwani serikali iko pamoja nao.

"Toeni ushirikiano yawezekana ni miundombinu ya jengo, lakini nawaambia Serikali itahakikisha inaimarisha miundombinu ya jengo hilo,"amesema Mbunge huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news