DC Mboneko akagua miradi ya maji

NA MARCO MADUHU

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maji Kata ya Solwa na Lyabukande wilayani Shinyanga, huku akiwataka wananchi waitunze miundombinu ya maji.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, (kushoto) akifungua maji katika kijiji cha Mwashagi, (kulia) ni Diwani wa Lyabukande Luhende Kawiza.

Amefanya ziara hiyo leo Septemba 7,2022, kwa kukagua utekezaji wa Mradi wa Maji Safi na Salama, katika Kijiji cha Mwandutu Kata ya Solwa na Kijiji cha Mwashagi Kata ya Lyabukande Miradi ambayo inatekelezwa na Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Shinyanga.

Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo, Mboneko amewataka waitunze miundombinu ya Miradi hiyo ya Maji, ili idumu kwa muda mrefu kuwahudumia na kuondokana na adha ya matumizi ya maji machafu.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na wanawake wa kijiji cha Mwandutu Kata ya Solwa wilayani Shinyanga, alipofanya ziara kukagua utekelezaji wa Mradi wa Maji kijijini humo.

"Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda sana wananchi wake, na ndiyo maana amekuwa akitafuta fedha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo hii ya maji, na anatekeleza ilani ya CCM kwa vitendo," amesema Mboneko.

"Nawapongeza pia wananchi kwa kutoa maeneo yenu na kupitisha mabomba ya maji, huu ndiyo uzalendo tunaoutaka, na muitunze miundombinu hii ya maji na kutoihujumu, na atakayeiharibu tutamchukulia hatua kali," ameongeza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kulia) akiendelea kukagua mabomba katika Tenki la Maji katika kijiji cha Mwashagi, (kushoto) ni Meneja wa RUWASA Emmael Nkopi.

Katika hatua nyingine Mboneko, amewataka wananchi wanapotaka kuunganisha maji majumbani mwao, wawatumie wataalamu na siyo kutumia vishoka.

Naye Meneja Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) wilayani Shinyanga Mhandisi Emmael Nkopi, amesema mradi wa maji katika kijiji cha Mwandutu asilimia kubwa umekamilika na utaanza kutoa huduma ya maji ndani ya mwezi huu.

Amesema Mradi wa Maji katika kijiji cha Mwashagi, wenyewe umekamilika na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akipiga picha ya pamoja mara baada ya kukagua mradi wa maji na Tenki katika kijiji cha Mwashagi.

Nao baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo, wameipongeza Serikali kwa kutekeleza Miradi hiyo ya Maji na kuwaondolea adha ya kutumia maji machafu pamoja na kutopoteza tena muda mrefu wa kufanya shughuli za maendeleo kwa sababu ya kufuata maji vijiji vya jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news