Balozi Luvanda:Mambo mazuri kutoka Japan yanakujaTanzania

NA DIRAMAKINI

LEO Septemba 7,2022 Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Baraka L.Luvanda amezungumza na waandishi wa habari kupitia mtandao wa Zoom.
Kupitia mkutano huo ambao umeratibiwa na Watch Tanzania umeangazi kwa kina kuhusu Diplomasia ya Uchumi na fursa mbalimbali ambazo zinaweza kutumika ipasavyo zikaleta matokeo chanya katika kustawisha uchumi wetu.

"Kumbukumbu zinaonesha kuwa misaada ya Japan kwa Afrika imeongezeka kutoka dola za Kimarekani bilioni 0.6 kwa mwaka 1993 hadi Dola za Kimarekani bilioni 20 mwaka 2009.

"Licha ya changamoto zilizopo wakati huu kama vile janga la Uviko, vita kati ya Ukraine na Urusi, mabadiliko ya tabianchi Serikali ya Japan bado imetoa kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 30 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2022 mpaka 2025 kwa nchi za Afrika ili kuziwezesha kutekeleza programu na miradi ya maendeleo itakayochochea mageuzi ya kiuchumi.
"Kwa kuhakikisha kuwa matumizi ya nishati ya salama na rafiki kwa mazingira Japan itazindua Mpango wake wa Japan's Green Growth Initiative with Afrika na kutoa Dola za kimarekani bilioni 4 za kutekeleza mpango huo kupitia vyanzo vya serikali na sekta binafsi.

"Japan kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika itafadhili kiasi kinachofikia Dola za kimarekani Bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha ustawi wa maisha ya watu wa Afrika, hii itahusisha mikopo mipya ambayo itafikia Dola za kimarekani bilioni 1 kwa lengo la kuleta mageuzi na matokeo chanya kwenye usimamizi na udhibiti endelevu wa madeni Barani Afrika.
"Japan imetoa kiasi kinachofikia Dola za kimarekani Bilioni 1.08 kupitia Global Fund ili kupambana na Uviko ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo, huu ni mkakati ambao Serikali ya Japan inaichangia Afrika katika dhana ya Usalama wa binadamu ikiwa ni jukumu lake la msingi.

"Mpango wa kuhamasisha maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika kwa kuwajengea uwezo vijana wa Afrika kwenye sekta ya viwanda, afya, elimu, kilimo, sheria, na utawala inakadiriwa vijana zaidi ya laki tatu watanufaika na mpango huo.
"Japan imeahidi kuendelea kufanya mapitio ya sheria zake za masuala ya usafiri iliyotokana na tahadhari ya magonjwa ya kuambukiza hususani Uviko kutoka nchi za Afrika ili kutanua wigo wa mwingiliano wa shughuli na watu kati ya Japan na Afrika, kulegezwa kwa masharti hayo kutawezesha programu za mafunzo yaliyokuwa yamesitishwa kufanyika ana kwa ana nchini humo kuanza tena na tayari makundi mbalimbali ya Tanzania yataanza kuingia Japan kuanzia Septemba na Oktoba mwaka huu.

"Japan itaendelea kusaidia kuimarisha amani barani Afrika ili iweze kutelekeza rasilimali zake katika shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia wakimbizi walio kwenye kambi mbalimbali katika nchi hizo ili waweze kujikwamua kimaisha, kujitegemea na kuendesha maisha yao wenyewe.

"Na pia Japan itamteua mjumbe maalum katika pembe ya Afrika kwajili ya kusimamia masuala ya usalama na amani katika eneo hilo.
"Japan kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa kiasi kinachofikia Dola za kimarekani Milioni 300 kwa ajili ya kuendeleza kilimo barani Afrika pamoja na kusaidia Mpango wa kujengewa uwezo watu laki mbili kwenye sekta ya Kilimo kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula.

"Kupitia mpango wa maendeleo ya kilimo barani Afrika, Serikali ya Japan imeahidi kuisaidia Tanzania Dola za Kimarekani laki tano kwa ajili ya kununua chakula kwa lengo la kukabiliana na baa la njaa nchini kufuatia athari za Uviko na vita kati ya Ukraine na Urusi.
"Tanzania imechaguliwa kuwa nchi ya mfano miongoni mwa nchi za Afrika na Shirika la Kimaendeleo la Kimataifa la Japan (JAICA) katika mpango wake kuimarisha kilimo cha uzalishaji wa mpunga barani Afrika.
"Japan imekubali ombi la Tanzania la kuongeza uwekezaji wake nchini pamoja na shughuli za kibiashara hivyo viongozi hao wamekubaliana kupitia Balozi zilizopo Dar es salaam na Tokyo kufanya ufatuliaji wa karibu kwa lengo la kubaini maeneo ambayo yana fursa za uwekezaji wa kibiashara,"amefafanua Balozi Luvanda.
"Japan imeishukuru Tanzania kwa kufanyia marekebisho sheria za kodi ambayo imewezesha kusainiwa kwa miradi mitatu ya Arusha Holili ule wa Kigoma na Zanzibar ambao utekelezaji wake umeanza.
"Japan imeiomba Tanzania kushirikiana katika kupaza sauti na kuzikemea nchi ambazo zinatumia nguvu zao za kiuchumi na fedha kuzinyonya nchi masikini na zile zinazoendelea.,"ameongeza Balozi Luvanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news