'Kusudio la kuhamia Dodoma halikuwa kuwatanguliza wadogo na baadhi ya wakubwa kusalia Dar'

NA ADELADIUS MAKWEGA

KATIKA matini yangu iliyopewa jina la Mashine Mara Tatu nilimsimulia kijana wa bodaboda niliyeficha jina lake ambaye alinieleza uhodari wa makampuni ya Wachina yanayojenga katika Mji wetu wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Kijana huyu alisema bayana kuwa makampuni haya yanatumia tekinolojia za kisasa, yanajenga saa 24 na mwisho yanalipa vibarua wake wanaofanya nao kazi katika ujenzi huo kwa wakati bila dhuluma, huku kijana huyu alizitaja Wizara ya Elimu, Wizara ya Maliasili na Wizara ya Maji kuwa spidi za ujenzi wake niwenye kasi nzuri machoni mwa wapita njia.

Binafsi baada ya kijana huyu wa bodaboda kuondoka zake nilijaribu kujiuliza je kuna faida zipi kama makampuni yaliyopewa dhamana ya kujenga majengo katika eneo la Mji wa Serikali kama yatamaliza ujenzi huo na kuyakabidhi majengo kwa wakati?

Jambo hili nilitafakari kwa siku kadhaa na kupata majibu mengi;

Kuipiga vizuri mbiu yangu ya mgambo ya majengo yote ya Serikali kukamilika kwa wakati, ifahamike kinagaubaga kuwa katika ujenzi huo fedha za umma za Watanzania zimeingizwa ili kuhakikisha makao makuu yanakamilika na kila mtumishi awe mkubwa au mdogo anakuwa na pahala pa kufanya kazi na kutoa huduma hiyo kwa Watanzania wanaohitaji huduma kutoka kwa serikali yao wakitokea kona zote za Tanzania iwe Kusini, Kaskazini,Mashariki au Magharibi na kufika kitovuni Dodoma.

Ifahamike wazi kuwa kusudio la kuhamia Dodoma halikuwa ni la kuwatanguliza wadogo Dodoma na baadhi ya wakubwa kusalia Dar es Salaam bali kila mmoja kuhamia Dodoma. 

Watumishi hao wa umma waliohamishiwa Dodoma bila ya kujali vyeo vyao kwenda Dar es Salaam au mikoa mingine ya Tanzania basi hilo lingekuwa ziara na siyo vingenevyo.

Kinyume chake ile dhana na muangua nazi, mkwezi anakwenda kuiangua halafu nazi inafika mapema kabla ya mkwezi hii haipaswi kuwa na nafasi katika dhana ya kuhamia Dodoma.

Kubwa kabisa kama taasisi zote za umma zikiwa eneo moja itasaidia wahitaji wa huduma kupata huduma kwa urahisi bila ya kuhangaika. 

Jambo hilo litasaidia kupunguza gharama za mafuta, gharama za safari za kutoka maeneo yalipangishwa majengo kwenda majengo ya awali.

Katika utafiti wanagu mdogo katika ofisi ambazo taasisi za umma zimepanga katika majengo ya binafsi au ya umma jijini Dodoma nimebaini sehemu kubwa la sakafu ya ghorofa moja inapangishwa kati ya shilingi 20,000,000-30,000,000/- kwa mwezi na upangaji huo unategemea mno idadi ya watumishi wanaopanga katika jengo hilo ndiyo kusema kama taasisi ina wafanyakazi wengi inaweza kupanga hata sakafu mbili za ghorofa kwa hiyo kwa mwezi mmoja wanaweza kulipa kodi ya zaidi shilingi milioni 60 za Kitanzania na kwa miezi 12 inaweza kulipa shilingi 720,000,000/-.

Katika utafiti wangu nilibaini kuwa mathalani taasisi moja ikiwa inapokea pesa ya uendeshaji kwa mwezi shilingi 500,000,000/- kwa mwaka itakuwa na zaidi ya bilioni 7 kama itatumia shilingi milioni 720 kama pango ndiyo kusema karibu asilimia 10 ya fedha yote ya uendeshaji wa taasisi kwa mwaka inatumika kwa pango tu.

Ukichukua kiasi hicho ukukazidihs kwa taasisi 10 itakuja bilioni zaidi ya saba zikitumika kulipa pango tu. Kiasi hicho ni kikubwa mno kingeweza kusaidia kufanyika kwa kazi kadhaa za taasisi za umma badala ya kulipa kodi.

Siamini kama pesa hiyo iwe milioni 720 au milioni 360 kama inatolewa na hazina itatoka nje ya bajeti ya taasisi iliyopangiwa, wataitoa wapi pesa hiyo? Ndiyo kusema kibubu cha bajeti iliyopangiwa taasisi hiyo itatumika na kuipa mzigo mkubwa taasisi hiyo tu na kuzikwamisha kazi zilizopangwa katika mpango kazi wa mwaka.

Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa wa majengo yote ya taasisi za umma na wizara zote Mji wa Serikali kukamilika haraka ili kuokoa pesa hizo na kama kuna mtu, taasisi iwe ya umma au binafsi itakwamisha/atakwamisha hilo lazima iwajibike/ awajibike katika hilo. Viongozi wenye mamlaka kama Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais waseme kwa herufi kubwa katika hilo.

Kuchelewesha kukamilisha ujenzi huu binasfi ninaona anayekwamisha anawajibu wa kulipia gharama hizo. Kinyume chake ni kuwabebesha Watanzania mzigo ambao haupaswi kuubeba.

Ukiweka kando hoja ya gharama tu hata kama taasisi zote zikiwa pamoja katika Mji wa Serikali itasaidia kupunguza gharama za kusafirisha nyaraka kutoka eneo moja kwenda lingine lakini pia itasaidia kupunguza gharama za usafiri na mafuta ya magari.

Isitoshe watendaji wa umma wakiwa pamoja Jijini Dodoma watajenga udugu na kufahamiana katika masuala ya kiutendaji na mambo ya kijamii.

Kwa hakika kwa sehemu kubwa watumishi na taasisi zote za umma zinazopaswa kuwepo makao makuu kama zikiwa Dodoma jambo hili litasaidia mno kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na kusaidia jiji hilo kupumua na habari ya vingora kuwa Dodoma na biashara zitashamiri zaidi Dar es Salaam.

Majengo ya Mji wa Serikali yakikamilika yatasaidia mno kujenga udugu, umoja na ushirikiano baina ya viongozi wa wizara na watumishi wao mathalani waziri muda wote awe Dar es Salaam wakati watumishi wengine wapo Dodoma, inawezekana watumishi wengi hawawezi kumfahamu waziri wao, utendaji wake wa kazi, dira yake na taasisi inapoelekea. 

Kama wakubwa wakiwa jirani na wafanyakazi wa chini jambo hilo linasaidia hata kiongozi mkubwa akipewa majukumu makubwa zaidi watumishi wanaweza kuwa mawakala wa kuelezea namna wanamfahamu kiongozi huyu na wataweza kumsemea vizuri kwa jamii ya Watanzania.

“Huyu anaweza kuifanya kazi hiyo aliyopewa kwa kuwa hata alipokuwa waziri wetu alifanya kazi vizuri.” Kinyume chake kama akipewa mtu ambaye yupo mbali nao “Huyu alikuwa Dar es Salaam muda wote wala hatumfahamu kabisa.”

Kwa mfano kuna siku nilikutana na mlinzi mmoja wa wizara iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyefanya kazi kipindi na marehemu Rais Benjamin Mkapa alipokuwa Waziri wa Habari, alisema bayana kuwa Mkapa hakuwa na shida na watumishi waliokuwa wakijituma kwa kazi huku akiwepo ofisini kwake muda mwingi na hata alipokuwa akisafiri wizarani palibandikwa tangazo kuwa waziri wao yupo pahala fulani kwa kazi fulani.

Kuhamia Dodoma lazima kusemwe kwa herufi kubwa hasahasa na viongozi wetu wakuu Rais mheshimiwa Samia suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu mheshimiwa Kasimu Majaliwa Majaliwa na sisi Watazania tunapaswa kuikuza sauti hiyo ili iweze kusikika na kila mmoja wetu awe mkubwa au mdogo kwa kufanya hivyo manufaa yote niliyoyataja hapo juu yatasaidia taifa letu.

Inafahamika wazi kuwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais wote hawa wana ofisi zao Dar es Salaam na Dodoma na katika kila mkoa wana Ikulu Ndogo wao wanaweza kufanya kazi maeneo yoyote ya taifa letu.

Wengine wote watakaoendelea kubakia Dar es Salaam wakae huko kwa gharama zao zisiwe gharama za serikali tangu makaazi, mafuta ya magari na gharama zingine isipokuwa kama watakuwa na kazi za kiserikali zinatambulika na taasisi husika.

Ninaiweka kalamu yangu chini hapo ya kulipiga chapuo la kuhamia Dodoma kwa wakubwa na wadogo nia kuchapulisha sote tuhamie Dodoma kwa kusema kuwa hoja ya kuhamia Dodoma ni ya kila mtumishi wa umma bila kujali ngazi yake, hamia Dodoma ni wakubwa na wadogo.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news