Rose Vicent alivyopita katikati ya tanuru la moto akiwa mtendaji wa kata, sasa ni Mbunge

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWAKA 2014 aliajiriwa kama Afisa Mtendaji katika Halmashauri ya Mbozi wakati huo ikiwa ni wilaya ya mkoa wa Mbeya lakini baadae wilaya ya Mbozi ikawa ndiyo makao makuu ya mkoa mpya wa Songwe wakati huo ukiongozwa na mheshimiwa Chiku Galawa.

Mtendaji huyu alifanya kazi katika kata kadhaa zikiwemo Vwawa, Hasanga na Hasamba katika vipindi tofauti.

Utaratibu wa Halmashauri ya Mbozi wakati huo, madiwani, baadhi ya watumishi wa wilaya hii na viongozi wakuu kiwilaya walikuwa wakizunguka katika kata hizo kupokea kero za wananchi, hilo kwa uhakika lilikuwa jambo zuri sana.

Lakini ndani yake baadhi ya viongozi wakitumia vikao hivyo kuwa mwiba wa kuwachoma, kuwajeruhi na kuwapunguza kasi baadhi ya watumishi wa umma waliokuwa na moyo thabiti lakini wakipinga baadhi ya tabia za baadhi ya wanasiasa wasio na nia njema.

Katika kata moja kulikuwa na walimu, wauguzi, matabibu, maafisa kilimo, maafisa mifugo na watendaji wa vijiji na kata huku kiongozi mkubwa wa siasa kwa kata ni diwani na mara moja moja wabunge walipita huko.

Mtendaji huyu wa kata alihimiza shughuli kadhaa za maendeleo katika kata hizo za Hasanga, Vwawa na Hasamba na wakati huo Songwe ni mkoa mpya na kata hizo ni kata zilizo hatua chache na makao makuu ya mkoa huu wa Songwe.Mkoa upate maendeleo unahitaji viongozi wenye juhudi sana siyo viongozi wa kuziba nafasi tu.

Miongoni mwa shughuli alizohimiza ilikuwa ni ujenzi wa zahanati ya eneo la Old Vwawa, malengo yalikuwa siyo vizuri Hospitali ya Wilaya ikapokea hata wagonjwa wenye matatizo madogo madogo, ni vizuri wagonjwa hao kupata huduma kutoka zahanati na ndiyo waende kituo cha afya, hospitali ya wilaya, mkoa au rufaa pale inaposhindikana na kutokufanya hivyo ni kuzibebesha mizigo hospitali ya juu na maelekezo ya kutibiwa ni wajibu kila mgonjwa kuanza kupata huduma kutoka katika zahanati. 
 
Kwa hiyo wakaazi wa Old Vwawa waliwajibika kujenga zahanati yao kinyume chake waliwajibika kutibiwa katika zahanati ya Mlowo na maeneo mengine.

Mtendaji huyu alihimiza ujenzi huo kwa kukusanya matofali, mawe, vifaa kadhaa na pesa taslimu na ujenzi huo kuanza mara moja. Kwa kuwa wakati huo serikali ilikuwa ikihimiza ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za kieletroniki jambo hilo lilisaidia kila mtendaji wa kata na vijiji kuwa na mashine ya kukusanyia mapato ya halmashauri husika vizuri sana.

Utaratibu wa kukusanya mapato kupitia mashine ulisadia mno pesa za serikali kuingia moja kwa moja katika mifumo ya kibenki huku jambo hilo la watendaji wa vijiji na kata kusimamia mapato likikumbwa na changamoto kadhaa. Baadhi ya wanasiasa walitamani mashine hizo kupatiwa watu wanaowaweza na kuwataka wao kwa manufaa yao.

Kumbuka utaratibu wa viongozi wa wilaya kuzunguka katika kila kata uliendelea kama kawaida na siku wakafika katika kata aliyekuwepo mtendaji huyu na kukuta ujenzi wa zahanati ukiendelea vizuri kabisa, walipouliza baadhi ya wanasiasa juu ya ujenzi wa zahanati hiyo walisema kuwa hawafahamu lolote juu ya ujenzi huo wa zahabati hii ya Old Vwawa.

Maamuzi yaliamuliwa mtendaji huyo apokonywe mashine ya kukusanyiwa mapato na kuwekwa kolokoloni muda huo huo mbele ya wananchi na watumishi wa kata hii aliyokuwa akiiongoza.

Polisi hawakuwa na shida yoyote wao walipokea maelekezo tu kutoka kwa waheshimiwa sana walikuwapo katika mkutano huo wa hadhara. Mtendaji huyu alipata msukosuko mkubwa kwa sababu mbalimbali kwanza hulka yake ya kujiamini, pili jinsia yake ya kike huku baadhi ya wanasiasa wakishangazwa na tabia hii ya mwanamke kujiamini mno mbele ya wanaume.

Wakati haya yanafanyika mwanakwetu hakuwepo lakini haya niliyakuta yakiendelea mwisho mwisho nilipochunguza mwisho wa siku mtendaji huyu hakuwa na kosa lolote lile. 
 
Alirudi kazini bila ya kukata tamaa, huku akihimiza wanakijiji wa Old Vwawa kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ambapo mwanakwetu alikutana na mtendaji huyo uso kwa uso huko huko Old Vwawa.

Kwa hakika wananchi wa Mbozi ni wapenda mno maendeleo japokuwa changamoto ni siasa za baadhi ya viongozi wa eneo hilo, mtendaji huyo alipata ushirikiano na kukamilisha zahanati hiyo lakini haikuwa hekima kubakizwa kufanya kazi eneo hilo na kuhamishiwa kata ya Hasamba.

Akiwa Hasamba mtendaji huyu wa kata alifanya kazi nzuri sana ya kukusanya mapato kwa kuwa kata hii ilitengeneza matofali mazuri ya kuchoma yaliyonunuliwa kila kona hadi Tunduma na Mbeya hivyo mapato mengi yalipatikana kutokana na chanzo hicho kilichosimamiwa vemana mtendaji huyu.

Baadaye mwanakwetu nilibaini kuwa wengi waliompinga mtendaji huyu hodari walichukizwa na uhodari wake wa kazi, kujiamini kwakwe na shida ya walio wengi wanadhana kuwa mtumsihi wa umma mwenye cheo kidogo ana anawajibu wa kuitikia ndiyo katika kila jambo.Je hiyo ni kweli?

Kwa hakika mtumshi wa umma anapaswa kuwa mtii kwa mambo ya msingi lakini siyo udhalimu na uovu. Kwa kupinga udhalimu na uovu kunaweza kuhatarisha nafasi yake, ajira yake na hata uhai wake lakini niseme tu ni heri ya usalama wa roho kuliko kuwa na usalama wa mwili.

Utendaji kazi wa mtendaji huyu wa kata unadhihirishwa hata sasa kwa kuwa zahanati ya Old Vwawa nimeambiwa inatoa huduma ya tiba kwa wakaazi wa eneo hilo ikiwa na watumsihi kadhaa na kuwapa nafasi ya kupata huduma ndogo ndogo hapo hapo jirani na makaazi yao.Natambua baadhi wakaazi wapya wa Old Vwawa wanaweza wasimkumbuke mtendaji huyu, lakini wanapokwenda kupata huduma katika zahanati hiyo wanapaswa kumkumbuka mtendaji huyu ninayemsimulia.

Mwanakwetu maisha yanasonga na hayarudi nyuma, mwaka 2020 mtendaji huyu wa kata ya Hasamba aligombea ubunge wa viti maalumu kupitia CCM katika mkoa wa Geita na kushinda kwa kura nyingi sana na hivi sasa ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akifahamika kama mheshimiwa Rose Vicent .

Inawezekana mheshimiwa Rose Vicent ni mbunge ambaye siyo maarufu sana katika bunge letu lakini leo mwanakwetu ninakuuma sikio kuwa Rose Vicent ni mwanamke hodari, mchapakazi, anayejiamini, anayefahamu analolifanya, siye wa kuitikia ndiyo kwa kila jambo, mwenye kuheshimu ndoa yake na mwanasiasa makini mno.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news