MABAO 13: Yanga, Simba SC zajipigia tu CAF

NA GODFREY NNKO

KLABU ya Yanga na Simba zote za jijini Dar es Salaam nchini Tanzania zimejikusanyia alama sita kila moja katika michuano ya Kimataifa huku ushindi huo ukisindikizwa na mabao 13.
Ushindi huo ni furaha kwa Watanzania wote ambao licha ya kila mmoja kuwa na timu yake, linapokuja suala la Kimataifa huwa wanaungana kuombeana heri waweze kusonga mbele. Kwani, ushindi wa namna hii si kwa klabu husika bali kwa Watanzania wote.

Kimetokea nini

Septemba 18, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Simba SC kupitia mshambuliaji Mzambia, Moses Phiri dakika ya 29 na 50 aliiwezesha kunyakua alama zote tatu.

Ni kupitia mtanange wa aina yake dhidi ya Nyasa Big Bullets ya nchini Malawi iliyoambulia mikono mitupu katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-0 kufuatia kushinda 2-0 pia kwenye mchezo wa kwanza Septemba 10, 2022 katika dimba la Bingu jijini Lilongwe nchini Malawi.

Kupitia mwalimu wa muda, Juma Mgunda wekundu hao walifanikiwa kutwaa alama tatu kwa mabao washambuliaji Mzambia, Moses Phiri kwa tik-tak dakika ya 28 na mzawa, John Bocco dakika ya 84.

Yanga SC je?

Wakati huo huo, Yanga SC ilifanikiwa kwenda Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini.

Ni kupitia mtanange wa aina yake wa marudiano uliopigwa Septemba 17, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Saalam.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Farid Mussa Malik dakika ya 47 na washambuliaji, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 58 na Fiston Kalala Mayele ambaye alifunga mabao matatu dakika za 60, 63 na 66.
Kwa sasa,Yanga SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 9-0 baada ya kuichapa Zalan 4-0 kwenye mechi ya kwanza wiki iliyopita.

Mambo yalikuwa hivi, katika mtanange huo ambao ulipigwa ndani ya Dimba la Benjamin Mkapa dakika 45 za awali zilitamatika kwa miamba hiyo ya soka kwenda mapumziko wakiwa na matokeo tasa.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga SC kupiga mpira wa nguvu ambao uliwawezesha kuimiminia Zalan FC kutoka nchini Sudan Kusini mvua ya mabao.

Ikumbukwe kuwa, chini ya Kocha wa Yanga, Prof.Nasreddine Nabi alipokwenda mapumziko aliwapa mbinu mpya za kuibuka na ushindi.

Alianza Mayele dakika ya 47 kutupia bao ambalo liliwanyanyua mashabiki wa Yanga SC katika viti huku dakika ya 55 Feisal akitumbukiza bao la pili.

Mabao yaliyofuata ni ya Mayele ambapo hadi dakika tisini zinatamatika katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga SC ilijizolea alama tatu ikiwa na mabao manne.

Nini kinafuata

Yanga SC katika raundi ya mwisho ya kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanakwenda kumenyana na Al-Hilal FC ya Omdurman nchini Sudan.

Ni baada ya Al-Hilal kuitoa St George ya Ethiopia kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ambapo mechi ya kwanza jijini Addis Ababa, St. George ilishinda 2-1, kabla ya Septemba 18, 2022 kuchapwa 1-0 mjini Omdurman, hivyo Al Hilal walisonga mbele kwa faida ya bao walilopata Ethiopia.

Wakati huo huo Simba SC itachuana na Primiero do Agosto ya Angola katika raundi ya mwisho ya kuwania kucheza Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Primiero de Agosto ya Angola ilifika hatua hiyo kwa kuitoa Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 1-0 ugenini wiki iliyopita na sare ya 1-1 nyumbani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news