Mchakato wa marekebisho ya sheria ya habari umefikia hatua nzuri-Msigwa

NA MWANDISHI WETU

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Bw.Gerson Msigwa amesema, mchakato wa marekebisho ya sheria zinazosimamia sekta ya habari nchini umefikia hatua nzuri.

Ametoa kauli hiyo alipoulizwa na mwandishi wa habari hii kuhusu hatua iliyofikiwa ya marekebisho ya sheria ya habari tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alipoagiza sheria hizo zifanyiwe marekebisho ili kuondoa vifungu vinavyolalamikiwa na wadau kuwa ni kandamizi.

Msemaji huyo ameeleza kwamba, Serikali inaendelea na maboresho ya mapendekezo hayo kabla ya kupelekwa bungeni na kwamba, wadau wa habari wataeleweshwa hatua inayofuata baada ya ile ya kikao cha pamoja kilichofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 12 Agosti, 2022.

Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza mamlaka husika kukaa pamoja na wadau wa habari ili kupitia vipengele vinavyolalamikiwa na hatimaye kupata muafaka wa pamoja.

Tayari serikali ilitekeleza ushauri wa serikali wa kukutana na wadau tarehe 11 na 12 Agosti mwaka huu, ambapo kikao hicho kilifanikisha makubaliano ya baadhi ya vipengele huku vichache kati yao vikiwa bado havijapatiwa mwafaka.

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza tarehe 26 Agosti 2022 alisema, serikali itaandaa kikao kingine ili kupitia vipengelea ambavyo hawajakubaliana na wadau.

"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Alifafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.

"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana,"alisema Mheshimiwa Nape.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news