Mhe.Othman:Tunahitaji ushirikiano katika Uchumi wa Buluu,uhifadhi na ufugaji nyuki

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ushirikiano wa karibu unahitajika kati ya Serikali ya Zanzibar na Australia katika kuzitumia vyema fursa za kiuchumi zilizopo kama njia ya kuwakomboa kimaisha.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo wakati akizungumza na Balozi wa Australia nchini Tanzania,Mheshimiwa Luke Williams, aliyefika ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali ya kuendeleza ushirikiano.

Amesema kuwa, yapo mambo yanayoshabihiana katika nchi hizo mbili na kwamba ushirikiano wa karibu ikiwemo kubadilishana ujuzi ni wa muhimu ili kuleta tija katika uzalishaji.
“Uchumi wa Buluu, uhifadhi wa mazingira ya bahari na ufugaji wa nyuki, ni maeneo muhimu sana ambayo ikipatikana nguvu ya mashirikiano, basi Zanzibar itapiga hatua katika kukamilisha azma ya serikali na kuzalisha ajira zaidi kwa wananchi,”amesisitiza Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Akielezea kuhusu ufugaji wa nyuki, Mhe. Othman amesema Zanzibar inazalisha asali nzuri sana ya nyuki wanaofugwa katika mikandaa ila kutokana na kukosekana kuitangaza na masoko ya uhakika basi fursa ya kipato inapungua.

“Tumeona zipo bidhaa nyingi ambazo zinazalishwa nchini kwetu, lakini kutokana na uhifadhi na namna duni ya kuzitangaza zinakosa masoko, ila ukizikuta namna zilivyohifadhiwa katika masoko makubwa kama ya nchi ya Dubai na kwengineko na zinavyokuwa na thamani kubwa zaidi, tunaona ni wazi ipo haja ya kuwa na mazingira mazuri ya elimu ya uhifadhi na kuzitangaza ili kulilinda soko letu la ndani.”
Mheshimiwa Othman amesema Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inapelekea sehemu kubwa ya ardhi kuliwa na bahari jambo ambalo ni hatarishi kwa maisha ya baadaye. Hivyo, ameomba msaada wa kitaalamu juu ya namna bora ya kupambana na tatizo hilo.

Aidha ameeleza kuwa jamii inapaswa kujiepusha na ukataji miti kiholela na badala yake kujikita kupanda miti na kuhifadhi mazingira hasa ya fukwe ili kuepusha tatizo hilo.

Aidha, Mheshimiwa Othman amesema taasisi zinazohusika na utamaduni hazina budi kuhakikisha wanautangaza utamaduni wa nchi kwa kupitia matamsha makubwa ya kimataifa ili kuitumia fursa hio kuitangaza nchi na utamaduni wake, sambamba na kumuomba Balozi wa Australia kuangalia namna na kuisaidia Zanzibar katika hilo.
Balozi Luke amesema nchi yake ipo tayari kuendeleza mashirikiano pamoja na kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbalimbali kwani nao ni wadau wakubwa wa utamaduni.
Katika ujumbe wake, Balozi Luke ameambatana na Mke wake, Bi. Hellen Luke, na msaidizi wake, Bw. Lewisi Hirst.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news