Mheshimiwa Sagini aguswa na Maonesho ya Kimataifa ya Biashara mkoani Mara, awapongeza TCCIA

NA FRESHA KINASA

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama mkoani Mara Mheshimiwa Jumanne Sagini, ametoa pongezi kwa viongozi wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo TCCIA Mkoa wa Mara kwa kuandaa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa yaliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi.

Mheshimiwa Sagini akitazama bidhaa za mjasiriamali katika Maonesho ya Mara International Expo alipotembelea maonesho hayo leo Septemba 9, 2022. (Picha na DIRAMAKINI).

Mheshimiwa Sagini amesema kuwa, hatua hiyo imesaidia kuzitangaza fursa na vivutio vya Mkoa wa Mara ziweze kutambulika zaidi kitaifa na Kimataifa. Na pia ni sehemu ya vijana kujifunza ujasiriamali na kujiajiri katika kuwasaidia kujipatia kipato chao na kumudu kuendesha maisha yao.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Septemba 9, 2022 akiwa katika maonesho hayo katika Uwanja wa Mukendo uliopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara ambapo pia alitembelea mabanda mbalimbali ya wafanyabiashara na wajasiriamali na kujionea bidhaa zao.

Mheshimiwa Sagini amesema, licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa maonesho hayo ya Kimataifa kufanyika mkoani Mara, lakini yamekuwa yakipekee kwani yamewezesha kujengwa mabanda zaidi ya 200 ambapo kila banda lina watu zaidi ya watatu na hivyo kuwezesha watu zaidi ya 600 walioweza kuleta biashara zao katika mabanda hayo jambo ambalo linatakiwa kuwa endelevu kwa kila mwaka.

Uendelevu wa maonesho hayo Mheshimiwa Sagini amesema, itapunguza makundi ya vijana ambayo yangeweza kufanya vitendo vya kihalifu katika jamii, na badala yake watapata ujuzi na maarifa ya kufanya biashara kujikwamua kiuchumi na kuimarisha amani na utulivu na hivyo vitendo vya kihalifu kupungua.

Aidha, Mhe.Sagini wakati akiendelea na zoezia la ukaguzi wa mabanda hayo, aliweza kutembelea banda la Maliasili na Utalii na kuwaomba kuwa mfano kwa kupanda miti na kuwafundisha wananchi namna ya kilimo bora na utunzaji wa Mazingira kwa Maendeleo endelevu ya kuifanya Tanzania izidi kuwa ya kijani.

Pia Mheshimiwa Sagini amesisitiza utunzaji wa mazingira ikiwemo milima ya Kyanyari na Buturu inayopatikana wilayani Butiama kama sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa kielelezo bora kkatika utunzaji mazingira na upandaji wa miti katika kulinda uoto wa asili na hivyo nyazo za Mwalimu zifuatwe kwa ufanisi.

Pia, amewaomba viongozi wa TCCIA Mkoa wa Mara, awamu ijayo na kuendelea ni vyema maonesho hayo yaandaliwe Wilaya nyingine kama sehemu ya kuleta chachu ya maendeleo ndani ya mkoa wa Mara na isiwe Musoma mjini peke yake, kwani lengo ni kuijenga Mara yenye uchumi mkubwa na kwa kupitia maonesho hayo itasaidia kuleta maendeleo zaidi ya kiuchumi na kijamii

Mheshimiwa Sagini akiteta Jambo na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Kilimo na Wenyeviwanda Mkoa wa Mara (TCCIA), Boniphace Ndengo. (Picha na DIRAMAKINI).

Boniphace Ndengo ni Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, kilimo Viwanda Mkoa wa Mara ambapo amesema, maonesho hayo yataufanya Mkoa wa Mara ujulikane zaidi Kimataifa na hivyo kuwavuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza ndani ya mkoa huo na kuleta mageuzi chanya ya kiuchumi na kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news