'Msinyamaze kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia, pazeni sauti'

NA FRESHA KINASA

AFISA Maendeleo ya Jamii mkoani Mara, Neema Ibamba ameyataka mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali mkoani humo yanayotekeleza miradi ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia yaweke mkazo wa elimu kwa wanawake na watoto juu ya kupaza sauti zao kueleza vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa bila kunyamaza.
Ibamba amesema kuwa, elimu ni muhimu katika kuwezesha kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia iwapo itatolewa kikamilifu kwa makundi hayo sambamba na ushiriki wa jamii nzima kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Ameyasema hayo leo Septemba 22, 2022 wakati akizindua mradi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia maeneo ya uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambapo utatekelezwa na Shirika la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara.

Amesisitiza pia mashirika kuwa na mikakati madhubuti ya uendelevu wa miradi yanayotekeleza badala ya kutegemea wahisani pekee ambao si wa kudumu ili kuzidi kuleta ufanisi kwa jamii.

"Mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto una maeneo manane ambapo eneo la kwanza ni kuimarisha uchumi wa kaya hii ni muhimu sana kusaidia mapambano, pili mila na desturi hapa mila nzuri lazima ziendelezwe na mbaya ziachwe Kama ukeketaji, na tatu mazingira Salama hapa lazima yawe sawa kwa wote elimu zaidi ifikishwe kwa jamii,"amesema Neema Ibamba.

Amesema, Mkoa wa Mara vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vipo vikihusisha ukatili wa kingono, ukatili wa kiuchumi, ukatili wa kisaikolojia, ukatili wa kimwili pamoja na vitendo vya ulawiti na ubakaji. Hivyo juhudi za pamoja baina ya wadau, wananchi na Serikali zinahitajika kufanikisha juhudi za mapambano ya ukatili wa Kijinsia.

Ameongeza kuwa, ili kuwa na Maendeleo thabiti kuanzia ngazi ya familia lazima kumaliza vitendo vya ukatili wa Kijinsia pamoja na wazazi kujenga msingi bora kwa watoto kwa kujenga usawa ikiwemo Katika mgawanyo wa majukumu ili watoto wakue wakitambua usawa ni muhimu.

Pia, amewataka Wanawake kuendelea kuishi na waume zao kwa heshima amani na utivu na kutotumia lugha chafu pindi wanapopata mafanikio hali ambayo imekuwa ikichangia vitendo vya ukatili.
Meneja wa Shirika la VIFAFIO, Majura Maingu amesema, mradi huo utatekelezwa kwa miezi nane kuanzia Septemba 2022 hadi Aprili 2023 katika Halmashauri ya Musoma na Halmashauri ya Bunda na utagharimu shilingi milioni 37 ambapo utagusa maeneo ya mialo ambapo shughuli za uvuvi zinafanyika.

Amewaomba viongozi wa maeneo ambako mradi huo unatekelezwa watoe ushirikiano wa dhati kusudi mradi huo uweze kuleta matokeo chanya.

Mratibu wa Mradi huo Robinson Wangaso amesema mradi huo utahusisha utoaji wa elimu maeneo ya mialo, kuendesha mijadala ya pamoja na Wadau, kuendesha shughuli za michezo kupinga ukatili wa Kijinsia, kuunda klabu za wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wapinga ukatili wa Kijinsia pamoja na kuimarisha mifumo ya Serikali za mitaa ngazi ya vijiji na kata zinazohusika na kupinga ukatili wa Kijinsia.
Wangaso amesema kuwa, matokeo ya mradi huo yanatarajiwa kuwa ni pamoja na kuwezesha Wanawake na watoto kuchukua hatua wanapofanyiwa ukatili wa Kijinsia pamoja na kuongeza ushiriki wa Jamii katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

Post a Comment

0 Comments