NDANI YA KOKWA LA EMBE-3:Usajili wa kisasa…

NA LWAGA MAMBANDE

KLABU au timu shiriki katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, msimu huu zinajivunia kufanya mambo ya kipekee zaidi.

Ni kutokana na uongozi husika kuwajibika kwa namna yoyote kuhakikisha fedha zinatafutwa na kuwekwa mezani ili kupata wachezaji mahiri.

Wachezaji hao wamekuwa wakisakwa iwe popote hapa Tanzania au kwa kuvuka mipaka. Wengine wamelazimika kutumia mamilioni ya fedha kunasa saini ya mchezaji mahiri ambaye wanaamini anaweza kuleta matokeo chanya katika timu.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anasema kuwa, hii ni hatua njema ambayo inadhirisha namna ambavyo soka la Tanzania linazidi kukuwa kwa kasi, ni kutokana na ukweli kuwa, mashabiki wa soka Tanzania huwa wanafurahi zaidi pale timu zao zinapopata matokeo bora, hivyo kuwekeza ni njia ya kupata kilicho bora,endelea hupitia shairi hapa chini;


1. Ligi yetu soka letu, linahamasisha hasa,
Ukiona timu zetu, usajili wa kisasa,
Na wageni huku kwetu, wengi wafurika hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

2.Geita Gold pia, huko ni dhahabu hasa,
Nafasi mejipatia, hapa lazima kuasa,
Nje kutushindania, wasijefanya makosa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

3.Wachezaji washeheni, tena wazoefu hasa,
Ukichungulia ndani, mwaka jana walitesa,
Mfungaji bora ndani, acheze bila ya visa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

4.Nawarudia Namungo, jinsi watia hamasa,
Hawa wanayo malengo, na uwanja wa kisasa,
Ni ya kurudi mipango, kimataifa kutesa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

5. Walicheza Afrika, na tena bila makosa,
Pazuri walipofika, ile mara moja hasa,
Ni kama tena wataka, hiyo nafasi kunasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

6. Wamefanya usajili, tena ni mzuri hasa,
Nchini na hata mbali, kandarasi si garasa,
Waweza kufika mbali, kama kikomaa hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

7. Ihefu natajataja, nayo yao kwasakwasa,
Kushuka kwao si hoja, wamekuja upya sasa,
Hii ligi ngojangoja, jinsi watavyotikisa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

8. Wadhamini wadhamini, wa kuwasifia hasa,
Tuseme bila ya soni, mpira kubwa fursa,
Timu cheki mifukoni, mingi inajaa pesa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

9. Wako wengi wadhamini, wachache nataja hasa,
Ambao wamethamini, hizi timu zetu hasa,
Chama cha mpira ndani, chaongoza kisiasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

10. Azam wewe Azam, metengeneza fursa,
Kila mtu ana hamu, ya kwamba udumu hasa,
Matangazo twafahamu, udhamini bora hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

11. NBCii asante, hatukufanya makosa,
Kwamba tenda uipate, ligi iwe ya kisasa,
Wafanya timu zipete, zote ziwe za kisasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

12. Wadhamini kila timu, wa zamani na wa sasa,
Kazi yenu ni muhimu, jinsi mnatoa pesa,
Twadhani na kwenu tamu, tangazeni vuna pesa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news