NDANI YA KOKWA LA EMBE-5:Sasa mbili mara mbili…

NA LWAGA MWAMBANDE

PONGEZI za kipekee kwa kila klabu au timu ambayo inawaza kufanya makubwa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika soka.

Kila mmoja anafahamu fika kwamba, soka ni ajira na ajira hii inanawiri zaidi pale ambapo timu husika inashinda na kutwaa mataji, vivyo hivyo ushindi ndio unatengeneza burudani kwa mashabiki.
 
Ni wazi kuwa, bila ushindi mengi huwa yanaibuka, yenye kufariji na wakati mwingine yenye kukatisha tamaa. Hilo lipo wazi, ndiyo maana timu inayofunga idadi kubwa ya mabao ndiyo mshindi.

Ikiwa timu zote hazijafunga bao au kuna idadi sawa ya mabao, mechi itatoka sare. Huku kanuni za mashindano zikielekeza kuwa,timu itakayoshinda baada ya mechi ya sare au sare ya nyumbani na ugenini, taratibu pekee zinazoruhusiwa kuamua timu itakayoshinda ni kanuni ya mabao ya ugenini.

Tayari tuna wawakilishi wetu katika michuano ya Kimataifa, huku mashabiki wa soka wakiwa na imani kubwa kwao,wanahitaji ushindi mnono ili kufikia lengo la kutwaa mataji, ndiyo maana mshairi wa kisasa Bw.Lwaga Mwambande akaamua kutumia muda wake kukumbushia jambo kupitia shairi hapa chini, endelea;

1. Ona toka timu mbili, za kimataifa hasa,
Sasa mbili mara mbili, Afrika twatikisa,
Hicho kipimo kamili, mpira wakua hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

2. Hapa shangwe shangilia, hii timu Simba hasa,
Kuibeba Tanzania, kisoka ya juu hasa,
Wametuwakilishia, kwa mfululizo hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

3. Pointi lizokusanya, Afrika imetikisa,
Hata nchi kuifanya, itishe hata kugusa,
Namungo vema kufanya, tuna timu nne sasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

4. Klabu bingwa ziko mbili, shirikisho mbili sasa,
Huko zikifanya kweli, pointi ni nyingi hasa,
Zitende siyo kauli, kushikilia fursa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

5. Yanga bingwa sanya pointi, kubebwa wewe makossa,
Simba zidi jizatiti, weka mpya ukurasa,
Mpira wekeni kati, nusu fainali hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

6. Geita Gold asante, umetumia fursa,
Huku kufanya upete, bila kufanya makosa,
Komaa upitepite, tafuta bora madesa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

7. Biashara ka Geita, iliipata fursa,
Ikashinda na kupeta, bila kufanya makosa,
Kwa Simba jenga ukuta, kimataifa lisusa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

8. Azam na timu yenu, usajili bora hasa,
Kimataifa ni mbinu, acha kufanya makossa,
Huo uzoefu wenu, na Shirikisho tikisa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

9. Tutaonana mwishoni, ligi funga ukurasa,
Tuone hii thamani, usajili bora hasa,
Timu zile kileleni, zisizo mengi makosa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

10. Haki ndani ya uwanja, hiyo ni muhimu hasa,
Mbinu nje ya uwanja, zisiachie makossa,
Watu wapigane kwanja, haki iwe wenye pesa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments