Prof.Muhongo awashika mkono wakulima kufanikisha kiwanda cha kusindika alizeti

NA FRESHA KINASA

KIKUNDI cha Changamkeni kilichopo katika Kijiji cha Masinono Kata ya Bugwema Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara kimekamilisha malipo ya kufungiwa umeme kwenye kiwanda chao cha Alizeti kinachojengwa kijijini Masinono huku Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Prof. Sospeter Mhungo naye akiwa amechangia gharama za kufungiwa umeme kwenye kiwanda hicho.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo leo Septemba 9, 2022 ambapo imeeleza kuwa, zoezi hilo la kufungiwa umeme limekamilika ambapo mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo kwa kushirikiana nao amechangia gharama za kufanikiwa jambo hilo muhimu kwa wanakikundi hao na wananchi wote kwa ujumla.

"Mwaka 2020, Shirika la SHIMAKIUMU linalojishughulisha na Kilimo na Ufugaji ndani ya Wilaya yetu, lilikipatia Kikundi cha Changamkeni mashine ya kukamua mbegu za alizeti. Mashine hiyo ina thamani ya Shilingi Milioni 35, ina uwezo wa kukamua mbegu za alizeti kwa kiasi cha magunia 40 kwa siku.

"Shukrani za dhati zinatolewa kwa SHIMAKIUMU kwa ufadhili huo utakaofaidisha wana kikundi cha Changamkeni, na wakulima wengine wa alizeti ndani ya Bonde la Bugwema na kwingineko mkoani Mara.

"Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo alianza kampeni ya kushawishi uanzishwaji wa kilimo cha alizeti jimboni humo mwaka 2016, na kwa misimu mitatu mfululizo ya kilimo aligawa bure mbegu za alizeti kiasi cha tani 9.66. Msimu wa mwaka 2018/2019, Wizara ya Kilimo ilichangia tani 10,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa, wakulima ndani ya Bonde la Bugwema ndio wanaongoza kwa kilimo cha zao la alizeti ndani ya Mkoa wa Mara. Ambapo kikundi cha Changamkeni kinakusudia kulima ekari 500 za alizeti ndani ya Bonde la Bugwema.

Mazao mengine yanayolimwa kwa wingi na wakulima wa ndani ya Bonde la Bugwema ni mahindi, mpunga, dengu na pamba.

Huku wakulima wa Bugwema wanasubiri kwa hamu kubwa mradi kabambe wa umwagiliaji ndani ya Bonde la Bugwema. Mradi huo utaanza kwa ufadhili ya Serikali yetu.
Picha za mbalimbali juu zinamuonesha Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo akiwa ndani ya kiwanda kidogo cha kusindika mbegu za alizeti. Kiwanda hicho kitakachofunguliwa mwezi huu na kinajengwa kijijini Masinono, Kata ya Bugwema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news