Rais Dkt.Mwinyi:Utoaji haki ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi hapa nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema utoaji wa haki ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuashiria Uzinduzi wa Ofisi ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar, uzinduzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.(Picha na Ikulu).
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 17, 2022 katika uzinduzi wa Ripoti ya Mahitaji ya Mfumo wa Mahakama Zanzibar pamoja na Ofisi ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC-ZANZIBAR), hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Uwanja wa Ndege, Zanzibar.

Amesema, imani za wananchi zinategemea zaidi kuwepo kwa uadilifu wa watendaji wa vyombo vinavyosimamia utoaji wa haki, na akatumia fursa hiyo kubainisha uwepo wa watendaji wachache katika taasisi hizo wanaaojihusisha na vitendo vilivyo kinyume maadili na utawala bora.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akionesha Kitabu cha Ripoti ya Mahitaji ya Mfumo wa Mahakama Zanzibar, baada ya kuizindua rasmi leo katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja na kushoto kwa Rais ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Shaban na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe.Dk.Haroun Ali Suleiman na kulia kwa Rais ni Mratibu wa Kitaifa, Wakili Onesmo Olengurumwa.

Ametoa wito kwa viongozi vya watendaji wa vyomvo hivyo kuwa makini na waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili wananchi waweze kujenga imani na vyombo hivyo.

Dkt.Mwinyi amesema, mafanikio ya kuchumi yanategemewa sana kuwepo kwa misingi ya sheria pamoja na mfumo bora wa mahakama.

Aidha, alipongeza uamuzi wa kufungua Ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu hapa Zanzibar na kusema hatua hiyo itaongeza kasi ya mafanikio katika utekelezaji wa shughuli zake.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi alisema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuboresha Idara ya Mahakama, (hata kabla ya ripoti hiyo kutayarishwa), ambapo imeanzia na ngazi ya Mahakama Kuu, lengo likiwa ni kuimarisha utendaji.

Amesema, maboresha hayo yanahusisha eneo la rasilimali watu, rasilimali fedha, mfumo wa mtandao pamoja na upatikanaji wa vifaa na zana muhimu za kutendea kazi, ikiwemo vyombo vya usafiri.

Ametoa shukrani kwa viongozi na watendaji wa idara hiyo kwa utendaji bora wa kazi mbali na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amesema ripoti hiyo itatumika kwa ajili ya kuandaa mpango kazi wa miaka mitano, lengo likiwa ni kuwa na mahakama inayowajibika ili hatimaye wananchi waweze kujenga imani nayo.

Amesema, bado kuna tatizo kubwa la jamii kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, hususani katika kesi za udhalilishaji pamoja na upatikanaji au usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, na akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini kusaidia kuihamasiaha jamii kubadili mitazamo.

“Vyombo vya sheria ikiwemo Ofisi ya DPP pamoja na ZAECA wajipange vyema kuhusiana na kesi wanazofikisha mahakamani, wahakikishe zinakuwa na mashahidi, ili kuwepo mafanikio kunahitajika mashirikanao kati ya vyombo vyote na wadau wa mahakama,”amesema.
Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Sheria, Katiba na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema Wizara inalenga kujenga mahakama za kisasa za ngazi mbalimbali katika mikoa yote nchini, ili kuwawezesha watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Alisema, wizara itaiangalia ripoti hiyo kwa makini na kutekeleza yale yote yalio ndani ya uwezo wa Serikali ili kuwawezesha watendaji kufanya kazi zao katika mazingira bora zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news