Rais Samia kufungua Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kesho anatarajiwa kufungua Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA Secretariat) utafanyika kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 14, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Septemba 11, 2022 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uwekezaji, Viwnada na Biashara, Dkt.Ashatu Kijaji wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba 12, 2022 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mhamasishaji wa Wanawake na Vijana katika Biashara Barani Afrika kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

"Mkutano huo utafungwa rasmi Septemba 14, 2022 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Amesema, mkutano huo unalenga kuwakutanisha pamoja wanawake na vijana katika biashara kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, hii ni hatua ya kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika biashara na katika mchakato wa kuanzisha Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara inayoandaliwa na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa kushirikiana na nchi wanachama wa AfCFTA.

Amesema, mkutano huo wa siku tatu utaongozwa na kauli mbiu isemayo Wanawake na Vijana: Injini ya ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika “Women and Youth: The Engine of AfCFTA Trade in Africa’’.

Kauli mbiu ambayo amesema, inafafanua kwa usahihi jukumu kuu la wanawake katika Afrika na Uchumi wa Dunia na umuhimu wa kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki na kutumia ipasavyo fursa za biashara katika Eneo Huru la Biashara la Afrika ili kuongeza ajira na kukuza uchumi imara kwa Taifa na jamii kwa ujumla.

Aidha, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 500 ambao ni pamoja na viongozi mbalimbali wanawake katika ngazi ya marais, marais wastaafu, makamu wa rais, mawaziri wakuu.

Wengine ni wakuu wa taasisi mbalimbali za Kimataifa,watu mashuhuri,mawaziri wanaosimamia sekta za biashara na masuala ya jinsia na wanawake,vijana na wafanyabiashara.

"Sambamba na mkutano huo, kutakuwa na maonesho ya wafanyabiashara yatakayohusisha wafanyabiashara wanawake na vijana kutoka katika nchi 55 za Afrika.Mkutano huo wa wanawake na vijana katika biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika, ni mkutano wa kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

"Hivyo, kwa ujumla, mkutano huu utatoka na mapendekezo ya Kisera na Mikakati madhubuti ya kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana kutumia fursa zinazotokana na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji.

Katibu Mkuu AfCFTA

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Wamikele Mene amesema, wanajisikia faraja kuufanya mkutano huo katika ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema, wamefikia hatua hiyo kutokana na namna ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wanawake na vijana katika biashara barani Afrika kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Mene amesema, lengo la kufanya mkutano huo ni kwa ajili ya kubadilishana mawazo,kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wanawake na vijana barani Afrika ili kwa pamoja waweze kuzipatia ufumbuzi wa haraka.

Amesema, baada ya mkutano huo wanaamini watakuja na mkakati maalumu wa kuzishirikisha sekta za fedha ili kuona namna zinavyoweza kutoa kipaumbele katika biashara ambazo zinaendeshwa na kundi hilo kwa matokeo bora

“Hatuwezi kuona matokeo ya hicho tutakachojadili ndani ya siku moja au mbili,bali kupitia mazingira jumuishi ambayo tunayaweka ili kuhakikisha mafanikio yanakuwa makubwa katika biashara za wanawake na vijana siku za usoni,”amesema Mene.

Mada sita

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema,mkutano huo utajadili mada mbalimbali muhimu ikiwemo changamoto wanazokumbana nazo Wanawake na Vijana katika biashara za Mpakani (Reflecting on Challenges Women and Youth face in Cross Border Trade in Africa).

Pili ni namna ya kusaidia wanawake na vijana ambao ni kichocheo katika Sekta ya Ubunifu Barani Afrika (Supporting Women and Youth as Drivers of the Creative Industry in Africa);

Mada ya tatu ni juu ya namna ya kutumia nyenzo za kidigitali za biashara ili kuimarisha ushindani wanawake na vijana katika Soko la Eneo Huru la Afrika la Biashara (Leveraging Digital Solutions to Trade to Enhance Women’s and Youth’s Competitiveness in the AfCFTA Market).

Nne, ni namna ya kusaidia urasimishaji wa biashara za wanawake na wijana ili waweze kunufaika zaidi na Mkataba wa Eneo Huru (Women and Youth in Informal Cross Border Trade: Supporting the formalization of women and youth in trade for greater benefits under the AfCFTA).

Tano, ni majadiliano kuhusu Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Youth Roundtable on the AfCFTA Protocol on Women and Youth in Trade) naKuimarisha ushirikishwaji wa Wanawake na Vijana katika masuala ya kifedha (Promoting Financial Inclusion for Women and Youth in Trade).

AfCFTA

Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni eneo lenye jumla ya nchi 55 za Afrika zenye watu bilioni 1.2 na Pato la Taifa (GDP) la dola za Kimarekani trilioni 3.4 ambapo Tanzania ni mwanachama.

Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni utaratibu wa pamoja wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (African Union-AU) unaolenga kuchochea uchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama.

Lengo hilo litafikiwa kwa kufunguliana masoko ya biashara ya bidhaa na huduma kwa kuondoleana ushuru wa forodha (tariff) na kulegezeana masharti na taratibu nyingine zisizokuwa za kiushuru.

Aidha, utaratibu huo unalenga kufanya Bara la Afrika kuwa soko moja ambapo nchi hizo zitaweza kutangamanisha juhudi nyingine za mtangamano wa kibiashara na uchumi ambazo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimekwishaanzisha.

Matangamano hayo ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community-EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sourthern African Development Community-SADC) ambayo Tanzania ni mwanachama.

Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika ulitiwa saini katika Mkutano wa 10 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Machi 12, 2018 jijini Kigali, Rwanda.

Hadi sasa, jumla ya nchi 54 kati ya nchi 55 za Umoja wa Afrika zimeshasaini mkataba huo isipokuwa nchi ya Eritrea. Nchi ambazo zimeridhia mkataba huo ni nchi 43 kati ya 54.

Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo tayari zimesharidhia mkataba huo. Baraza la Mawaziri lilipitisha Waraka wa kuridhiwa kwa Mkataba huo tarehe 7 Agosti 2021 na Bungeni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likapitisha rasmi Azimio la kuridhia Mkataba huo mnamo tarehe 9 Septemba 2021.

Hatua ya Tanzania kuridhia Mkataba huo iliwasilishwa kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika tarehe 17 Januari 2022.

Mkataba huo ulianza kufanya kazi rasmi mwezi Mei 2019, ikiwa ni siku 30 tangu kukamilika kwa takwa la kisheria la Mkataba kuridhiwa na angalau nchi 22 (asilimia 40). Hii ni kutokana na matakwa ya Ibara ya 23 ya Mkataba wa AfCFTA.

Utekelezaji wa mkataba ulizinduliwa rasmi mwezi Julai 2019 jijini Niamey, Niger na nchi kukubaliana utekelezaji wake uanze tarehe 1 Julai 2020.

Lakini utekelezaji ulichelewa kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya maeneo ya majadiliano ambayo ni pamoja na Vigezo vya Uasili wa Bidhaa (Rules of Origin) ambavyo ni muhimu katika utambuzi wa asili ya bidhaa ikiwa ni pamoja na nchi inakotokea. Hivyo, hadi sasa bado biashara haijaanza kufanyika chini ya AfCFTA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news