SAUTI KENDA ZA WANANCHI:Ninauliza Waziri yupo? Waziri hayupo, Naibu Waziri naye yupo? Na yeye hayupo baba...lakini karani wake yupo. Katibu Mkuu yupo? Nayeye hayupo...

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIKU moja mwanakwetu alikuwa amekaa katika ofisi ya wizara moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika chumba kimoja kidogo sana chenye uwezo wa kukaa wasioozidi watu watano.

Akiwa hapo aliingia mtumishi mmoja akawa anamuuliza mambo kadhaa na na yeye akawa anamjibu ndugu huyu jambo moja baada ya jingine.
Picha na janicebastanicoaching.

Wakati anaongea na ndugu huyu ambaye alikuwa na mazungumzo marefu ya dakika kadhaa zilisikia sauti kadhaa za kelele kutoka nje ya jengo hili kwa mfano kijana wa usafi akisafisha vioo vya dirisha moja kubwa huku kelele za kugongagonga nje ya dirisha hilo.

Alipotazama aliona maji yakimwaga mwaaaaaaa…! katika dirisha la kioo na kisha kioo hicho kufutwa na kitambaa waa waa…! Masikio yake yalisikia sauti nyingine ya ngo ngo ngo…! lidriillll lidriillll lidrilili…!

Sauti hizo zilikuwa ni za fundi ujenzi akitimiza majukumu yake ya siku ipasavyo ili jioni alipwe ujira wake aweze kutunza familia yake, lakini kwa upande mwingine bila ya fundi huyu kujua kuwa kugonga huko ngo ngo ngo na lidrili lidrili lidrili ni kero kubwa kwa mtu anayefanya kazi katika ofisi kwa utulivu.Kwa kuwa maendeleo hayaji kwa utulivu bali msuguano.

Mwanakwetu alisikia sauti nne kutoka nje siku hiyo yaani; mwaaaa, waaa, ngo na lidriliii na sauti ya tano ilitoka ndani kwa bwana mkubwa huyu aliyeingia katika chumba alipo.

Mazungumzo na ndugu aliyefika ofisini nilipokuwapo yaliendelea vizuri huku kompyuta mpakato ya mwanakwetu ikilalamika tata tata tata kwa kugongwa herufi zake akikamilisha matini yake ya siku hiyo. Sauti ya herufi za vifungo vya kompyuta haikuwa na shida kwa mwanakwetu kwani mlio huo kauzoea sana.

Ofisi hii ilikuwa na mlango mmoja tu mgeni huyu aliyeingia alipo mwanakwetu alipita, masikio ya mwanakwetu yalikaribishwa na sauti mbili mpya za majibizano nje ya mlango huu huku zikisindikizwa na sauti ya kenda ya mvumo wa upepo wa Dodoma vuuuu ..! ambao ulisaidia mno mwanakwetu kusikilia kila kilichozungumzwa.

“Andika jina lako katika kitabu cha wageni, siandiki jina langu, nakuomba andika ili uweze kupata huduma na huo ndiyo utaratibu wetu. Ninauliza Waziri yupo? Waziri hayupo, Naibu Waziri naye yupo? Na yeye hayupo baba...lakini karani wake yupo. Katibu Mkuu yupo? Nayeye hayupo, naibu katibu mkuu yupo? Pia baba nayeye hayupo lakini yupo anayekaimu.

”Mwanakwetu alisikia maswali hayo yakiulizwa na kujibiwa. Kumbuka mwanakwetu yupo ofisini na hayo majibizano ya sauti mpya mbili anayasikia kupitia mlango wake.Hapa sasa anasikia sauti kenda kwa wakati mmoja; Mwaaaa, Waaa, Ngo, Lidriiii,suti za mgeni ndani ya ofisi alipo mwanakwetu, tata tata ya kompyuta, sauti za majibizano nje ya mlango na vuuu ya upepo.

Baba andika jina lako ukapate huduma ilisikika sauti ya mlinzi akimwambia mgeni nje ya mlango wa mwanakwetu.

Mabishano ya mlinzi na mgeni yalimvutia mwanakwetu lakini kuamka alipo kwenda kujua kinachoendelea zaidi ilikuwa ngumu sana, anamuachaje mgeni aliyepo ofisini? Umakini wa kuyasikiliza na kuyanasa kama sumaku mazungumzo haya haukuwa na budi.

Anafanyaje? Akakumbuka akiwa kijana mdogo anajifunza utangazaji na utayarishaji wa vipindi vya redio kwa wazee waliofanya kazi na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kama Suleiman Muhogora na Malima Ndelema walinifundishaga namna ya kuwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza sauti nyingi kwa wakati mmoja na kuelewa yote yanayozungumzwa katika sauti hizo kwa kuzipa umuhimu sauti moja baada ya nyingine. Huku wakimfundisha pia namna ya kuyanukuu maelezo ya watu neno kwa neno bila ya kuyaandika pahala popote.

Alilikumbuka darasa hilo na siku hiyo alilitumia vizuri sana somo hilo, mwanakwetu mabishanao yaliendelea na yule mgeni aligoma kuandika jina lake na wala kwenda kumuona karani wa Naibu waziri wala kaimu Katibu Mkuu na akaondoka zake.

Baada ya dakika kadhaa tu ndugu aliyekuwa naye ofisini mwanakwetu alitoka ndipo na mwanakwetu alipata upenyo wa kutoka hapo ofisini na kwenda kumuuliza yule mlinzi kuwa huyo mgeni alikuwa na shida gani? Mlinzi alisimulia kilichotokea kama kilivyo hapo juu. Aliongeza neno hili,

“Mimi ni mlinzi tu sina mamlaka yoyote hapa, mie ni bawabu tuu baba lakini alikuwa mkali kweli mgeni huyu” Mwanakwetu aliuliza ulichukua namba yake? Mlinzi alinjibu kuwa aligoma kuandika chochote kile. Mwanakwetu alitoa pole na kurudi ofisini.

Alipoketi alitafakari tukio hilo akasema kuwa kuna umuhimu wa viongozi wa umma na wenye dhamana kubwa kujitahidi kuwepo katika ofisi zao ili kuwapa nafasi Watanzania kusikilizwa kwa maana Watanzania ndiyo wenye hizo ofisi.

Mtanzania anapokwenda ofisini kwa kiongozi anaweza akawa na mambo kadhaa yawe ya wazi au ya siri, mambo hayo anaweza kuyasema kwa yule anayemuamini na aliyekabidhiwa dhamana tu na si kwa mtu mwingine.

Kama wizara ina waziri na naibu, katibu mkuu na naibu wake wajitahidi hata kama kazi ni nyingi lazima hao viongozi wawili wawepo ofisini hapo kutoa nafasi kwa wenye ofisi yao (wananchi) kupata huduma.

Kwa sasa viongozi wengi wa umma wanatumia vyombo vya habari kama ushahidi wa kazi wanazozifanya na mara nyingi zinakuwa mbali na vituo vyao vya kazi hilo si jambo baya lakini pia kuna wajibu wao kuwepo ofisini maana mambo ya siri hayawezi kusemwa hadharani.

Pia ofisi hizo kama makao makuu ya nchi ni Dodoma basi waheshimiwa hawa wapatikane Dodoma amabapo ndiyo makao makuu na kama hawapo katika vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu waulizwe wapo wapi ? Kama taasisi hizo zina ofisi zaidi ya moja ni vizuri kuwa na ofisi moja ambapo wote watapatikana kufanya utendaji wa kazi kuwa mzuri na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Kama kiongozi hayupo katika ofisi kwa safari zakitendaji au jukumu lolote la umma mbao za matangazo za taasisi hiyo zibandike taarifa hiyo, yupo wapi na kwa kazi gani kwa kufanya hivyo kutaboresha utendaji wa kazi kwa wakubwa na hata kwa watumishi wa chini.

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news