Sekta ya Madini yadhamiria kufanya makubwa

NA TITO MSELEM

MKURUGENZI wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini Augustine Ollal amesema Wizara ya Madini inaendelea na mchakato wa kuhuisha Sera ya Madini ya Mwaka 2009 baada ya kugundua inamapungufu.
Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ililenga kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa na kuondoa umaskini kwa kufungumanisha sekta nyingine za uchumi.

Hayo yamebainishwa na Ollal wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuhuisha Sera ya Madini ya Mwaka 2009 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Ollal amesema uhuishaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 unapitia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Mwaka 2009 na ushirikishwaji wa wadau kutoka ndani na nje ya wizara ambapo kwa sasa wizara ipo katika hatua ya awali ya kutathmini Sera ili kujua changamoto za utekelezaji wake.
Aidha, Ollal amesema Serikali kupitia marekebisho ya Sheria ya Madini Sura 123 yaliyofanyika Mwaka 2017 imeweka utaratibu wa Makampuni kuwajibika kwa jamii na ushiriki wa watanzania katika utoaji wa huduma na bidhaa migodini.

“Katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi 2022, migodi 13 ilitoa jumla ya shilingi bilioni 16.08 kwa ajili ya miradi ya afya, elimu, maji, barabara na miradi ya kiuchumi katika Halmashauri za wilaya mbalimbali nchini,” amesema Ollal.

Ollal amesema Serikali imeendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika Sekta ya Madini ili kuongeza mchango wa sekta katika Pato la Taifa.

Pamoja na mambo mengine, Ollal amesema marekebisho ya Sheria ya Madini Mwaka 2017 yalilenga kutambua haki ya ushiriki wa Serikali katika shughuli zote za uchimbaji, uchenjuaji na umiliki wa hisa zisizopungua asilimia 16 katika makampuni ya uchimbaji.
Pia, Ollal amesema katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa madini, wizara imehamasisha taasisi za fedha nchini kutoa mikopo ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 36 zimekopeshwa kwa wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewasilisha Taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Mpango wa Serikali wa kuunda mkakati wa kuendeleza madini ili kuboresha na kuongeza ubora wa kuendesha shughuli za madini.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Danstan Kitandula ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Madini kuiwezesha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili iweze kufanya tafiti zaidi za kijiofizikia kwa skeli kubwa kwa lengo la kufikia zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 16 iliyopo sasa.

“Suala la utafiti linapaswa kupewa kipaumbele sababu roho ya shughuli za madini ni tafiti tukifeli kwenye shughuli za utafiti maana yake tutafeli kila sehemu kwenye shughuli za madini,” amesema Kitandula.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameishukuru Kamati hiyo kwa ushauri wake makini ambao umelenga kuhakikisha usimamizi wa Sekta ya Madini unakuwa wenye manufaa kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news