Sheria ya kulinda taarifa binafsi yaja

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Moses Nnauye amesema, Baraza la Mawaziri limeridhia kutungwa kwa sheria ya kulinda taarifa binafsi nchini.

Mheshimiwa Nape ameyasema hayo Septemba 7, 2022 wakati akifungua mkutano wa wadau wa mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA ) kwa maana ya Connect to Connect.

Waziri amesema kwa mara ya kwanza sheria hiyo itasomwa katika mkutano wa Bunge utakaoanza Septemba 13, 2022 jijini Dodoma huku akiwataka wadau watakaokuwa na nafasi za kutoa maoni wafanye hivyo.
 
Katika kongamano lililowakutanisha wadau wa TEHAMA wakiwemo wa miundombinu kutoka ndani na nje ya Tanzania,Mheshimiwa Waziri Nape amewataka wadau kutoa maoni huru yatakayopelekwa bungeni na kujadiliwa ili sheria itakayotungwa iwe bora na yenye kulinda taarifa binafsi za Watanzania.

Pia Mheshimiwa Waziri Nape amesema, kongamano hilo limetoa taswira chanya kwa Tanzania katika ramani ya Dunia hususani kwenye mabadiliko ya teknolojia kwa lengo la kujenga uchumi wa kidigitali.

Sambamba na kutatua changamoto za kimawasiliano huku akibainisha dhamira ya serikali ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika fursa zinazotokana na masuala ya teknolojia kwa sasa.

Post a Comment

0 Comments