'Panya road' kukiona cha moto

NA DIRAMAKINI

OPERESHENI maalumu ya kuwasaka nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa vijana wanaojihusisha na matukio ya uhalifu ambao wamejipa majina ya Panya Road jijini Dar es Salaam imeanza.

Hayo yamebainishwa na mmoja wa maafisa wa Jeshi la Polisi wakati akizungumza na DIRAMAKINI ambapo amesisitiza kuwa,wahalifu wa namna hiyo wanatambulika ndani ya jamii, hivyo wazazi wa vijana hao wasipokaa na kuwakanya watoto wao, operesheni hiyo ikiwapitia hakuna wa kulaumiwa.

"Hii ni operesheni shirikishi, na itakuwa nyumba baada ya nyumba, mtaa baada ya mtaa. Hatuwezi kuwavumilia watu ambao kwa maslahi yao wanawapa hofu, kuwajeruhi na kuwaibia wananchi mali zao, lazima kila mmoja awajibike,nipende kusisitiza kuwa, wazazi pia tuna jukumu kubwa la kuhakikisha malezi bora yanastawi kwa watoto wetu ili wasikumbane na kadhia hapo baadaye,"ameeleza Afisa huyo.

Hayo yamejiri baada ya vikundi vya uhalifu kurudi tena na kuvamia nyumba 24 za wapangaji wa Mtaa wa Kabaga Kinyerezi Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Dar es Saalam huku wakijeruhi na kupora mali za wananchi.

Wananchi walieleza tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 6, 2022 (saa 8 usiku) katika maeneo hayo ambapo raia wanne walijeruhiwa na kwa sasa wapo Hospitali ya Rufaa ya Amana wakipatiwa matibabu.

Kaimu Kamanda wa kanda hiyo, Wiliam Mkonda amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kuwa, "Taarifa za tukio hilo nilisha zielezea toka jana."

Aidha, Bw.Zahoro Juma ambaye aliyejeruhiwa na kuibiwa pikipiki mpya aina ya Boxer 125 alisema wakati wanakuja kuvamia eneo lao lenye nyumba 14 walikuwa vijana zaidi ya 30 huku wengine wakiwasubiri nje wakiwa kwenye bodaboda.

"Wakiwa wanapiga baruti, walianza kuvamia nyumba moja hadi nyingine kuvunja milango kujeruhi na kuchukua wanachokitaka, na watu waliokuwa wanapiga kelele kama akina mama wamejeruhiwa kwa kupigwa mapanga maeneo mbalimbali ya mili yao,"alisema Juma.

Naye Jakson Joseph aliyejeruhiwa kwa kupigwa mapanga kichwani mara tatu na miguuni alisema, vijana hao walikuwa wadogo na hatari kwa kuzingatia walivyomshambulia wakati anatoka ndani kwake kwa lengo la kutaka kwenda kumsaidia jirani yake.

Kwa upande wake, Hashimu Gulana ambaye ni mwenyekiti wa mtaa huo ameeleza kusikitishwa na tukio hilo huku akiwalaumu wananchi wa mtaa huo kushindwa kupigiana simu kuwadhibiti vijana hao waliodumu kwenye eneo hilo kwa saa mbili wakitekeleza vitendo hivyo ambapo baadaye maafisa wa jeshi la polisi walifika eneo la tukio.

Post a Comment

0 Comments