TANZANIA, DRC ZAAHIDI UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA MKUTANO WA JPC

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula na Waziri wa Mtangamano wa Kikanda na Nchi zinazozungumza Kifaransa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Didier Mazenga Mukanzu wamesisitiza umuhimu wa masuala yaliyoafikiwa katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) baina ya nchi hizo yanatekelezwa ipasavyo badala ya kuishia katika makabrasha.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mtangamano wa Kikanda na Nchi zinazozungumza Kifaransa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Didier Mazenga Mukanzu wakisaini Taarifa ya Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na DRC uliomalizika jana jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao wametoa kauli hiyo tarehe 14 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam wakati wanafunga mkutano huo wa JPC uliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022.

Mkutano huo wa JPC ulipitia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa pili uliofanyika nchini DRC mwaka 2002 na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano yatakayokuwa na tija na yanayoendana na hali ya sasa ya mabadiliko yanayoendelea duniani.

Mawaziri hao waliridhishwa na utekelezaji wa maazimio hayo, licha ya Mkutano huo kutofanyika kwa miaka mingi na kushuhudia katika Mkutano huo, nchi hizi mbili zikitiliana saini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya Ulinzi na Usalama.

Hati hizo zilizosainiwa na Waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Mhe. Stegomena Tax na Waziri wa Ulinzi wa DRC, Mhe. Gilbert Kabanda Kurhenga ziliainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa, mazoezi ya pamoja, mafunzo, utafiti na matibabu wakati wa operesheni za kijeshi.

Maeneo mengine ambayo mataifa hayo yamekubaliana na michakato ya kuwekeana saini baina ya nchi mbili inaendelea ni pamoja na: uendelezaji wa miundombinu ya usafiri wa reli, bandari, maji na anga; maliasili na utalii; biashara na uwekezaji; huduma za kifedha; kilimo; uvuvi; kupambana na ugaidi; biashara haramu ya binadamu; ufugaji na nishati.

Kuhakikisha makubaliano hayo yanatakelezwa kama ilivyokusudiwa, Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint Implementation Committee-JIC) imeundwa ambayo itakuwa inakutana kila baada ya miezi sita ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa Waheshimiwa Mawaziri kusaini taarifa ya mkutano na kutangaza kuwa Mkutano wa Nne wa JPC utafanyika nchini DRC mwaka 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news