Tanzania na Msumbiji zakubaliana kuendeleza ushirikiano

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wameshuhudia utiaji saini wa Hati mbili za Makubaliano (MoU) baina ya nchi hizo mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi kabla ya kuanza mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye Ikulu ya Maputo leo tarehe 21 Septemba, 2022.

Hati hizo ambazo zimelenga zaidi usalama na amani zimetiwa saini jijini Maputo, siku ya kwanza ya ziara ya kiserikali ya Rais Samia nchini Msumbiji.

Mkataba wa kwanza unaohusu Uratibu wa Huduma za Utafutaji na Uokoaji umetiwa saini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk pamoja na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Msumbiji, Mhe. Mateus Magala.
Makubaliano ya pili yaliyotiwa saini na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Mhe. Cristovao A. Chume yanahusu ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi.

Kutokana na kupungua kwa biashara na uwekezaji kutoka Shilingi bilioni 53,524.5 mwaka 2020 hadi Shilingi bilioni 46,006.00, Viongozi wote wawili wamekubaliana kutumia kila fursa hususan kwenye sekta za kilimo, uvuvi, mafuta na gesi pamoja na madini. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati akikagua Gwaride la Heshima mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Maputo leo tarehe 21 Septemba, 2022.

Nchi zote mbili zimehuisha mfumo wa kubadilishana wanafunzi ujulikanao kama (TAMOSE) ulioisha muda wake mwaka 2015 kwa kunufaisha wanafunzi 369, na kukubaliana kuongeza muda tena.

Vile vile, Rais Samia ameelezea kuwa Tanzania iko tayari kutengeneza mpango mkakati wa kuleta walimu nchini Msumbiji kwa ajili ya kufundisha lugha ya Kiswahili hasa kwa shule za msingi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania ukipigwa kwenye mapokezi rasmi yaliyofanyika katika Ikulu ya Maputo nchini humo tarehe 21 Septemba, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news